Breaking News

Serikali yapewa ushauri pato la Dola tril 1


WATAALAMU wa uchumi wameishauri serikali izingatie nguzo tatu za Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025-2050 ili kufikia lengo la nchi la kuwa na kipato cha kati cha juu na pato la Dola za Marekani trilioni moja ifikapo 2050.

Juni 14, mwaka huu wakati anazindua Bunge la 13 jijini Dodoma, Rais Samia Suluhu Hassan, alisema serikali itaanza utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025-2050 ikilenga kujenga Taifa jumuishi lenye ustawi, haki na linalojitegemea.

Rais Samia aliwaeleza wabunge dira mpya imeweka vigezo vya kuchagua sekta na maeneo ya kupewa kipaumbele yaliyobainishwa kwenye andiko la dira yenyewe. Alisema kati ya mikakati itakayofanyiwa kazi ni kuwekeza zaidi kwenye sekta zinazoajiri watu wengi na miongoni mwa sekta hizo ni kilimo, utalii, viwanda, ujenzi na madini.

“Malengo yetu ya kiuchumi ni kupandisha kasi ya ukuaji wa uchumi kutoka asilimia 5.6 ya sasa hadi zaidi ya asilimia 7 kuelekea mwaka 2030. Ukuaji huu utaiwezesha serikali kuboresha huduma za kijamii na kujenga miundombinu wezeshi ya kiuchumi,” alisema Rais Samia. Aliongeza: “Tutaimarisha masoko ya mitaji kwa kuhamasisha uwekezaji wa ndani, na kutumia rasilimali zetu kama madini kudhamini mikopo ya uwekezaji, badala ya kuweka mzigo mkubwa kwenye Deni la Taifa.

Mwelekeo wetu ni kukua kwa pamoja kwa uchumi unaogusa maisha ya mtu mmoja mmoja na uchumi jumla”. Hivi karibuni Mhadhiri na Mkuu wa Idara Msaidizi, Idara ya Masomo ya Biashara na Rasilimali Watu kutoka Chuo Kikuu Katoliki cha Mbeya (CUoM), Samson Mwigamba alisema anaamini miongozo iliyowekwa kwenye Dira 2050 ikizingatiwa lengo la Tanzania kuwa na uchumi wa kati wa juu na pato la Dola za Marekani trilioni moja litafanikiwa.

“Lazima tubadilishe fikra zetu, hatuwezi kufikia malengo hayo kama tutakuwa na fikra ya mali za umma hazina mwenyewe…badala yake kila mmoja ajitoe na hilo ili lifanikiwe lazima somo la dira lieleweke kwa kuanza na watumishi wa umma,” alisema

Mwigamba alipozungumza na HabariLEO. Aliongeza: “Dira inataka Tanzania iongoze kwa uzalishaji Afrika Mashariki na iwe miongoni mwa nchi 10 Afrika na duniani, lazima uwekezaji mkubwa kwenye kilimo ufanyike.” Mwigamba alisema ni muhimu sasa kwa vijana kufika elimu ya juu iwe kawaida na atakapomaliza imuwezeshe kufanya kazi mbalimbali kisomi na si kutembea na bahasha ya vyeti kutafuta kazi.

Pia, alisema ni muhimu serikali iruhusu ufanyaji kazi saa 24 kama ilivyoruhusu usafiri wa mabasi mikoani. “Kwa nini tusifanye kazi saa 24? Hatuwezi kufika tunapotaka kama hatufanyi kazi saa 24, China wanafanya hivyo na sasa unaona wanashindana uchumi wao na Marekani,” alisema Mwigamba.

Mtaalamu wa siasa, Ally Mkimo alisema ili kufikia malengo ya Dira 2050 ni lazima uchumi uwe imara, jumuishi na shindani. Mkimo alisema kama pato la Dola za Marekani trilioni moja litafikiwa maana yake uchumi wa mwananchi mmoja mmoja utakua kutokana na kunufaika kupitia mipango ya uwezeshwaji.

“Nchi ikifika kwenye pato hilo maana yake pato litakuwa limeongezeka kutokana na uzalishaji na kwa sababu hiyo wananchi watakuwa wameajiriwa kwenye maeneo hayo ya uzalishaji na rasilimali zitakuwa zikiwanufaisha wanachi,” alisema. Aliongeza: “Kama sekta zile chochezi zilizotajwa kwenye dira kama usafirishaji fungamanishi zitakuzwa maana yake sekta hiyo inakwenda kugusa wananchi wengi.”

Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (SAUT), Dk Isack Safari alisema ni muhimu kuimarisha kilimo kwa kukifanya cha kisasa. “Tuwe na viwanda vya kuhusiana na kilimo vitakavyotengeneza vitu vya kutumika kwenye kilimo mfano trekta, tuwe na viwanda vyetu wenyewe Watanzania wenyewe watengeneze ziende kwenye kilimo tusitegemee kuagiza nje,” alisema Dk Safari.

Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk Paul Loisulie alisema ni muhimu kufanya ushirikishwaji wa wadau wote katika maeneo yao ili wajione wanamiliki mchakato wa kufikia matarajio hayo. “Pia, ni muhimu kufanya usimamizi madhubuti kwa watumishi wa umma ambao ndiyo injini ya uendeshaji na kuhakikisha kwamba nchi inaweka mikakati ya kukusanya mapato ya kutosha ili kuwezesha utekelezaji,” alieleza Dk Loisulie.

Hivi karibuni Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba alitaja mambo ya kuzingatia ili kufikia lengo la kuwa na uchumi wa dola za Marekani trilioni moja. Dk Mwigulu alisema dira hiyo ni kielelezo cha matarajio ya Watanzania ambao wanataka nchi yao ifikie uchumi wa kati wa Dola za Marekani trilioni moja ifikapo mwaka 2050.

“Hatuwezi kufikia uchumi wa Dola trilioni moja kwa kuendelea kuuza bidhaa ghafi au kufanya mabadiliko kidogo tu. Inatutaka tuwe na mbinu bunifu zenye tija tuwe na njia mpya za kufanya mambo, tuanzishe kampuni mpya, tuwe na bidhaa mpya na teknolojia mpya zinazoweza kukua mara 10 badala ya asilimia 10,” alisema.

Aliongeza: “Inahitaji tuje na ubunifu wa Kitanzania utakaovutia mataifa na kuzalisha masoko ya nje. Inawezekana kabisa, twendeni tuunganishe nguvu” 



No comments