Simba yafunguka kocha mpya
KLABU ya Simba imesema itatumia kipindi cha mapumziko kupisha ratiba ya michuano ya fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) zinazotarajiwa kuanza Morocco Desemba 21, mwaka huu kutafuta kocha wa kuinoa timu hiyo.
Simba ambayo iliachana na Meneja wake Mkuu, Dimitar Pantev iko chini ya kocha Selemani Matola akikamilisha ratiba ya mechi za Ligi Kuu leo kwa kuikabili Azam, Uwanja wa Benjamin Mkapa kabla ya kwenda mapumziko.
Akizungumza na HabariLEO hivi karibuni, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally alisema watatumia kipindi cha mapumziko kupisha michuano ya Afcon kutafuta kocha atakayekuja kukinoa kikosi chao.
Alisema kwa sasa timu hiyo itakuwa chini ya kocha Selemani Matola kwa muda mpaka pale mchakato wa kumpata kocha mpya utakapokamilika kipindi hiki cha mapumziko kupisha michuano ya Afcon.
“Matola atamalizia mechi yetu ya leo dhidi ya Azam na baada ya hapo tutatumia kipindi hiki cha mapumziko kusaka kocha mpya,” alisema Ahmed.
Aidha, Ahmed alielezea dhamira yao ya kufanya vizuri kwenye michuano ya ndani na ya kimataifa msimu huu licha ya kuanza vibaya kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.
“Tumeanza vibaya michuano ya Ligi ya Mabingwa lakini hii sio mara ya kwanza kwetu, tuliwahi kuwa kwenye hali kama hii lakini msimu huu tumepania kufanya vizuri kwenye mashindano ya ndani na ya kimataifa,” alisema Ahmed.
Simba imepoteza mechi zake mbili za Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kufungwa bao 1-0 na Petro de Luanda, Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam kabla ya kukubali kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Stade Malien, Bamako, Mali.
No comments