Breaking News

TAASISI 9 ZANZIBAR KUWASILISHA TATHMINI YA UCHAGUZI MKUU MKUU 2025 KESHO.



Na Mwndishi wetu.

Taasisi zinazotetea haki za wanawake, vijana, watu wenye ulemavu na watoto Zanzibar kesho Jumamosi tarehe 06 Disemba 2025 zitaungana kwa pamoja kuadhimisha Siku 16 za Kupinga Udhalilishaji wa Kijinsia katika hafla maalum itakayofanyika katika Ofisi za TAMWA Zanzibar, Tunguu. Katika hafla hiyo itawasilishwa ripoti ya maoni ya wadau juu ya kuangalia nafasi ya mwanamke katika uchaguzi mkuu uliopita kwa mtazamo wa usawa wa kijinsia ikiwemo ushiriki jumuishi na wenye usawa kwa makundi yote katika mfumo wa kisiasa ambapo itaangalia mafanikio, changamoto na mwenendo wa haki za wanawake, vijana na watu wenye ulemavu katika mazingira ya kisiasa na ya kidijitali. Hafla hii inatarajiwa kuwakutanisha wadau 80 kutoka taasisi za kiserikali, zisizo za kiserikali, pamoja na waandishi wa habari kwa lengo la kuongeza uelewa na kuimarisha mbinu za pamoja za kukabiliana na udhalilishaji wa kijinsia katika zama za mabadiliko ya teknolojia na taarifa.Taasisi zinazoanda maadhimisho haya ni Jumuiya ya Wanawake Wenye Ulemavu Zanzibar (JUWAUZA), Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar (ZLSC), Pamoja Youth Initiative (PYI), Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA), Jumuiya ya Mazingira, Jinsia na Utetezi Pemba (PEGAO), Jumuiya ya Kupambana na Changamoto za Vijana Zanzibar (ZAFAYCO), Jukwaa la Vijana Zanzibar (ZYF), Mtandao wa watetezi wa haki za binaadam Tanzania (THRDC) pamoja na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania,Zanzibar (TAMWA ZNZ). Mikataba mbalimbali ya kimataifa ambayo Tanzania ikiwemo Zanzibar imeridhia inasisitiza kulinda na kuendeleza haki za wanawake na watoto, mikataba hiyo ni pamoja na Mkataba wa Kutokomeza Aina Zote za Uonevu Dhidi ya Wanawake (CEDAW), Itifaki ya Maputo inayotetea haki za wanawake barani Afrika; Azimio la Beijing (1995) linalosisitiza ushiriki wa wanawake katika uongozi, pamoja na Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), hususan Lengo namba tano linalolenga usawa wa kijinsia na kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na wasichana. Ujumbe wa Kimataifa kwa mwaka 2025 ni “TUUNGANE Kukomesha Ukatili wa Kidijitali Dhidi ya Wanawake na Wasichana”, huku ujumbe wa kitaifa ukiwa “Mitandao Salama ni Haki: Maliza Ukatili wa Kimtandao kwa Wanawake na Watoto.” Ujumbe huu unasisitiza umuhimu wa kuhakikisha matumizi salama ya teknolojia, kuimarisha mifumo ya kudhibiti na kuripoti ukatili wa mtandaoni, na kulinda haki za wanawake na wasichana kwenye majukwaa ya kidijitali. Kampeni ya Siku 16 ni harakati ya kimataifa iliyoanzishwa mwaka 1991 inayolenga kuhamasisha hatua za kukomesha ubaguzi na ukatili wa kijinsia. Maadhimisho huanza tarehe 25 Novemba, Siku ya Kimataifa ya Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake, na kuhitimishwa tarehe 10 Disemba siku ya Haki za Binadamu Duniani huku ikisisitiza kwamba udhalilishaji wa kijinsia ni ukiukwaji wa haki za Binadamu. Kampeni hii huhamasisha mabadiliko ya sera, elimu kwa umma, utafiti na hatua za pamoja za kukomesha ukatili wa kimwili, kijinsia, kisaikolojia, kiuchumi na sasa ukatili wa kidijitali ambao unaongezeka duniani kote. Imetolewa na: Jumuiya ya Wanawake Wenye Ulemavu Zanzibar (JUWAUZA) Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar (ZLSC) Pamoja Youth Initiatives (PYI) Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA) Jumuiya ya Mazingira, Jinsia na Utetezi Pemba (PEGAO) Jumuiya ya Kupambana na Changamoto za Vijana Zanzibar (ZAFAYCO) Jukwaa la Vijana Zanzibar (ZYF) Mtandao wa watetezi wa haki za binaadam Tanzania (THRDC) Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ).


No comments