Breaking News

TAASISI ZA KUTETEA HAKI ZA WANAWAKE, VIJANA NA WATU WENYE ULEMAVU ZANZIBAR ZATOA TATHMINI YA NAFASI YA MAKUNDI MAALUM KATIKA UCHAGUZI 2025



Na Mwandishi wetu.

Taasisi zinazotetea haki za wanawake, vijana, watoto na watu wenye ulemavu Zanzibar zimeungana kwa pamoja kuadhimisha Siku 16 za Kupinga Udhalilishaji wa Kijinsia katika hafla maalum iliyofanyika katika Ofisi za TAMWA Zanzibar, Tunguu. 

Katika hafla hiyo, taasisi hizo zimewasilisha ripoti ya tathmini ya ushiriki wa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu katika Uchaguzi Mkuu wa 2025, ikilenga kuangalia usawa wa kijinsia, ushiriki jumuishi katika siasa na changamoto zinazoathiri makundi maalum katika nyanja za kisiasa na za kidijitali.

Akifungua mkutano huo, Mjumbe wa Bodi ya Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Zanzibar (TAMWA ZNZ), Mwatima Rashid, amesema asasi zinazopambana na udhalilishaji wa kijinsia zina jukumu muhimu katika kuhakikisha zinapaza sauti za makundi yaliyo hatarini. Amesema wanawake, watoto na watu wenye ulemavu wanahitaji ulinzi wa karibu ili waweze kupata haki zao bila vikwazo vinavyowakwamisha kushiriki kikamilifu katika maisha ya kijamii na kiuchumi.

Amesisitiza kuwa taasisi hizo zinapaswa kuongeza juhudi za utoaji wa elimu na uhamasishaji kuhusu masuala ya ukatili wa kijinsia, kwa kuwa uelewa wa jamii ndio msingi wa kujenga mazingira salama. Mwatima ameongeza kuwa mashirikiano ya karibu kati ya asasi za kiraia, viongozi wa serikali, wadau wa maendeleo na jamii kwa ujumla ni muhimu katika kutokomeza vitendo hivi ambavyo vinaathiri ustawi wa makundi maalum.

Aidha, ametoa rai kwa vyombo vya habari na watetezi wa haki za binadamu kuendelea kusimama kidete katika kuhakikisha matukio ya ukatili hayaachwi bila kutolewa taarifa na kufanyiwa kazi. Ameeleza kuwa kupitia sauti za pamoja na hatua madhubuti, Zanzibar inaweza kujenga jamii yenye usawa, inayoheshimu haki za kila mtu na kuhakikisha usalama wa makundi yote katika nyanja zote za maisha.



Akiwasilisha ripoti hiyo kwa niaba ya taasisi hizo, Mkurugenzi wa JUWAUZA, Sabah Ali Mzee, amesema ripoti hiyo imeonesha mafanikio kadhaa katika mchakato wa uchaguzi lakini pia imesisitiza changamoto zinazotakiwa kushughulikiwa kwa haraka, zikiwemo ukosefu wa rasilimali kwa wanawake wanaojitosa katika siasa, mazingira yasiyo rafiki kwa watu wenye ulemavu wakati wa uchaguzi, na ongezeko la vitendo vya udhalilishaji mtandaoni. Aidha, ametoa wito kwa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) na ile ya Bara (INEC) kuboresha huduma rafiki kwa makundi maalum.

Wito kwa Tume ya Uchaguzi Bara na Zanzibar kuongeza upatikanaji wa huduma rafiki kwa wanawake na watu wenye ulemavu katika uchaguzi ili masuala haya yatekelezeke kwa ufanisi,” alisema Sabah Ali Mzee.

Kwa upande wa vyombo vya dola, Inspekta wa Polisi kutoka Makao Makuu ya Polisi Zanzibar, Sadik Ali Sultan, alibainisha kuwa mapambano dhidi ya udhalilishaji yanahitaji nguvu ya pamoja na uwajibikaji wa jamii nzima.

Masuala ya udhalilishaji ni mtambuka na yanahitaji nguvu moja kuyashughulikia ili tuweze kuyapunguza au kuyatokomeza kabisa,” alisema Inspekta Sadik Ali Sultan.

kosa ya mtandaoni “Jamii inapaswa kutambua makosa yanayofanywa mtandaoni yana sheria yake, hivyo ni vyema anayefanyiwa makosa haya kuripoti katika vituo vya polisi ili sheria ifuate mkondo wake,” aliongeza.

Kiongozi wa dini, Rev. Lamec A. Byonge, alisisitiza umuhimu wa kuimarisha elimu kwa jamii ili kupunguza vitendo vya udhalilishaji.
Ni wakati sasa kuongeza juhudi ya utoaji wa elimu ya masuala ya udhalilishaji kupitia vyombo vya habari na maeneo mengine ikiwemo nyumba za ibada na shuleni ili kujenga jamii itakayoheshimiana,” alisema Rev. Byonge.

Maadhimisho hayo yamehudhuriwa na wadau kutoka asasi za kiraia, wawakilishi wa Serikali na makundi mbalimbali ya kijamii.


No comments