Breaking News

BANDARI YA SHUMBA KULETA MAGEUZI YA KIUCHUMI PEMBA.


Na Mwandishi wetu Pemba.

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Zanzibar, Dk. Khalid Salim Mohammed, ameonesha kuridhishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Bandari ya Shumba pamoja na jengo la abiria, miradi ambayo serikali inaipa kipaumbele kwa ajili ya kuimarisha uchumi wa wananchi wa Pemba na Taifa kwa ujumla.

Akizungumza mara baada ya kukagua mradi huo Kisiwani Pemba, Dk. Khalid amesema kukamilika kwa bandari hiyo kutafungua rasmi milango ya biashara baina ya Zanzibar na maeneo mengine, hususan Bandari ya Mombasa, hatua ambayo itachochea shughuli za kiuchumi.

  “Nimeridhishwa na kasi ya ujenzi unaoendelea hapa Shumba, kukamilika kwake kutatoa fursa ya uingizaji na utoaji wa mizigo kutoka Mombasa kwa urahisi zaidi,” amesema.

Waziri huyo ameongeza kuwa ujenzi huo utaongeza chachu ya maendeleo kwa wakazi wa Pemba, hasa wale wanaojishughulisha na biashara na usafirishaji wa bidhaa. “Bandari hii italeta mageuzi makubwa ya kiuchumi kwa wananchi na Taifa kwa ujumla,” alisema.



Akifafanua kuhusu dhamira ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dk. Khalid amesema mpango uliopo ni kuhakikisha bandari hiyo inaendeshwa kibiashara kikamilifu, ili kuongeza fursa za kiuchumi kwa wananchi na wawekezaji. “Azma ya serikali ni kuiona Bandari ya Shumba ikiendeshwa kibiashara ili wananchi na wawekezaji waweze kubadilishana bidhaa kwa urahisi na kupunguza gharama,” alieleza.

Aidha, Waziri amesema serikali inaandaa mpango mahususi wa kuhakikisha bandari hiyo inapokea boti za mwendokasi na boti za mizigo, ambazo zitasaidia kupunguza gharama za usafirishaji wa bidhaa kati ya Unguja na Pemba. “Tunataka boti za mwendokasi na mizigo ziwe zinapokelea hapa ili kupunguza gharama za usafirishaji na kusaidia kushuka kwa bei ya baadhi ya bidhaa,” alisema.

Dk. Khalid ameongeza kuwa mpango huo pia utachochea uhusiano wa kibiashara kati ya visiwa hivyo na bandari za nje. “Hatua hii pia itatoa fursa ya biashara kati ya Pemba na Mombasa kuimarika zaidi,” alisema.

Katika ziara yake, Waziri huyo pia alikagua ujenzi wa mradi wa uwanja wa ndege, ambapo alielezea kuridhishwa kwake kutokana na hatua za awali za ujenzi huo kuendelea kwa kasi na kwa ubora unaotakiwa. “Nimeridhishwa na kazi zinazofanyika katika uwanja wa ndege, hatua za awali zinaendelea vizuri sana,” alisema.

Kwa upande wake, Mkandarasi wa Jengo la Abiria katika Bandari ya Shumba, Mhandisi Alexander Chauruwi kutoka kampuni ya FELIX, ameomba serikali kuongezwa muda wa miezi minne ili kukamilisha ujenzi wa jengo hilo. “Tunaomba muda wa ziada wa miezi minne ili kukamilisha jengo la abiria ambalo litachukua abiria 450,” alisema.

Mhandisi Chauruwi alifafanua kuwa jengo hilo linahitaji matumizi ya vifaa maalum vya kiufundi, hivyo muda wa nyongeza utasaidia kuhakikisha mradi unakamilika kwa ubora ulioainishwa. “Tukipewa muda huu, tutahakikisha kazi inakamilika kwa ubora wa juu na kwa mujibu wa makubaliano,” alisema.

Wananchi waliokuwepo katika eneo hilo walionesha matumaini makubwa kwa mradi huo, wakisema kuwa utapunguza changamoto ya usafiri na biashara kati ya Pemba na maeneo mengine. Wametaja kuwa ushushaji wa mizigo utarahisishwa na bei za bidhaa zitashuka.



Miradi hii ya kimkakati inatajwa kuwa injini muhimu ya maendeleo ya kiuchumi kwa Pemba, na inaendana na dhamira ya serikali ya awamu ya nane chini ya Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi ya kuimarisha miundombinu ya usafiri baharini na angani.

Kwa ujumla, kukamilika kwa miradi ya Bandari ya Shumba na Uwanja wa Ndege kutafungua ukurasa mpya wa maendeleo, kuongeza fursa za ajira, na kuimarisha biashara kati ya Pemba na maeneo mengine ndani na nje ya nchi.





No comments