Breaking News

Baraza la Taifa la Michezo zanzibar Lapata Muundo Mpya wa Utendaji.

 


Na Said Khamis

Kamisheni ya Utumishi wa Umma imewasisitiza watendaji wa Baraza la Taifa la Michezo Zanzibar kuhakikisha wanaufanyia kazi muundo mpya wa Taasisi hiyo kwa kuzingatia sheria, taratibu na miongozo ya utumishi wa umma. 

Akizungumza wakati wa kukabidhi rasmi muundo huo ofisini kwake Mwanakwerekwe, Katibu wa Kamisheni hiyo, Kubingwa Mashaka Simba, alisema hatua hiyo ni mwendelezo wa jitihada za Serikali kuboresha utendaji katika taasisi zake ili kuongeza ufanisi na kuimarisha uwajibikaji.

Alifafanua kuwa kukamilika kwa muundo huo ni matokeo ya kazi kubwa iliyofanywa kwa ushirikiano kati ya Kamisheni na watendaji wa Baraza, na kwamba utakuwa dira muhimu katika kuimarisha utendaji wa taasisi hiyo. 

Katibu Kubingwa aliwahimiza watendaji wa Baraza hilo kutowasita kuwasiliana na Kamisheni iwapo watakutana na changamoto zozote za kiutendaji zinazohusiana na muundo huo, ili kupata ufumbuzi sahihi utakaowezesha utekelezaji bora wa majukumu yao.

Kwa upande wake, Mrajis wa Vyama vya Michezo Zanzibar, Abubakar Moh’d Lunda, aliishukuru Kamisheni kwa kukamilisha mchakato huo muhimu, akisema kuwa muundo mpya utaweka mwongozo thabiti kwa Baraza katika kusimamia vyama vya michezo na kuendeleza wanamichezo nchini. 

Alieleza kuwa ukosefu wa muundo kwa muda mrefu uliathiri uwajibikaji na utekelezaji wa majukumu ya Baraza, lakini sasa wana matumaini kuwa muundo huo utarahisisha kupanga safu za uongozi, kuboresha utendaji na kuendana na mkakati wa Serikali wa kuimarisha taasisi zake.


No comments