RAIS MWINYI :SMZ KUENDELEA KUTATUA CHANGAMOTO ZA WATU WENYE ULEMAVU NCHINI.
Na Siti Ali.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuchukua hatua za kimkakati kuhakikisha changamoto zinazowakabili Watu Wenye Ulemavu nchini zinapatiwa ufumbuzi wa kudumu.
Akizungumza leo tarehe 03 Desemba, 2025 katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Watu Wenye Ulemavu Duniani, yaliyofanyika katika Ukumbi wa Dkt. Ali Mohamed Shein, Tunguu, Mkoa wa Kusini Unguja, Rais Dkt. Mwinyi ametangaza kuwa Serikali itaendelea kuhakikisha Watu Wenye Ulemavu wanapata haki za kijamii, kisiasa, na kiuchumi bila ubaguzi. Alihaidi kuwa hakuna mlemavu atakayekosa fursa ya kujiendeleza katika jamii.
Aidha, Rais Dkt. Mwinyi ametaja hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali, akisema kuwa Serikali inazingatia mahitaji maalum ya Watu Wenye Ulemavu katika ujenzi wa miundombinu kama vile hospitali, skuli, ofisi za umma, na barabara. Kwa mfano, alisema kuwa Serikali imejenga skuli mbili maalum kwa wanafunzi wenye ulemavu katika Mkoa wa Kusini Unguja na Pemba, na kwamba inakusudia kujenga skuli nyingine tatu katika mikoa mingine.
kwa upande wa ruzuku Rais Dkt. Mwinyi ameeleza kuwa Serikali itaendelea kutoa ruzuku, vifaa saidizi, mafunzo, na mikopo isiyo na riba kwa Watu Wenye Ulemavu ili kuwasaidia kiuchumi na kujitegemea. Aliwahimiza wananchi na jamii kwa ujumla kuwasajili watoto wote wenye ulemavu ili waweze kupata vifaa bure kutoka kwa Serikali.
Sambamba na kutoa mikopo isiyo na riba kupitia Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (ZEEA) pamoja na fedha za uwiano kutoka Serikali za Mitaa kwa Watu Wenye Ulemavu ili kuwasaidia kuimarisha maisha yao.
Maadhimisho hayo huadhimishwa kila ifikapo Disemba 3 kila mwaka ambapo mwaka huu kitaifa imeadhimishwa katika mkoa wa Kusini Ungija.



No comments