Breaking News

SERIKALI YA AWAMU YA NANE KUTATUA CHANGAMOTO YA MAJI MKOA WA KASKAZINI UNGUJA

 


Na Nishan Khamis.

Wizara ya Maji, Nishati na Madini Zanzibar imewahakikishia wananchi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja kuwa Serikali ya Awamu ya Nane, inayoongozwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, imejipanga kikamilifu kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama katika mkoa huo.

Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Maji katika wizara hiyo, Mhandisi Jokha Salum Mohamed, kwa niaba ya Waziri wa Maji, Nishati na Madini, mara baada ya kufika katika Kijiji cha Mkwajuni, Wilaya ya Kaskazini A, kusikiliza kero na changamoto ya maji inayowakabili wananchi wa jimbo hilo.

Amesema serikali inatambua kikamilifu changamoto ya maji katika Mkoa wa Kaskazini Unguja na kwamba miradi mikubwa ya maji inayoendelea kutekelezwa na kukamilishwa italeta suluhisho la kudumu. Ameitaja mradi wa maji wa lita milioni tano unaoendelea kutekelezwa katika Kijiji cha Nungwi kuwa miongoni mwa miradi mikubwa itakayosaidia kuondoa tatizo hilo.

Mhandisi Jokha amewaomba wananchi kuwa na subira wakati serikali ikiendelea na jitihada za kukamilisha miradi hiyo, akisisitiza kuwa dhamira ya serikali ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji ya uhakika.

Kuhusu changamoto iliyosababishwa na kuondolewa kwa tanki la maji katika jimbo hilo, amesema amelichukua suala hilo na kulifikisha ngazi husika kwa lengo la kulifanyia kazi kwa maslahi mapana ya maendeleo ya wananchi wa jimbo la Mkwajuni, Mkoa wa Kaskazini Unguja na Zanzibar kwa ujumla.

Kwa upande wao, Mbunge, Mwakilishi na Diwani wa jimbo hilo wamesema kuwa ni takribani miaka kumi imepita tangu kuondolewa kwa tanki hilo, hali iliyosababisha wananchi wa jimbo na wilaya kwa ujumla kukumbwa na changamoto kubwa ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa muda mrefu.


Wamesema tanki hilo lilikuwa likihudumia maeneo mengi ya wilaya hiyo, na kuondolewa kwake kumeathiri zaidi wanawake ambao wamekuwa wakibeba mzigo mkubwa wa kutafuta maji. Viongozi hao wameiomba serikali kuchukua hatua za haraka ili kumaliza adha hiyo ya muda mrefu.

Nao baadhi ya wananchi wa Mkwajuni wamesema wanawashukuru viongozi wao kwa jitihada wanazochukua kushirikiana na serikali hadi wizara kufika moja kwa moja kusikiliza changamoto yao. Wamesema hatua hiyo ni ya kupongezwa na wameahidi kuendelea kushirikiana na viongozi wao katika shughuli mbalimbali za maendeleo ya jimbo hilo.


No comments