RAIS SAMIA: JENISTA MHAGAMA ALITANGULIZA MASLAHI YA TAIFA, AMEACHA ALAMA ISIYOFUTIKA
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa Marehemu Jenista Mhagama alikuwa akitanguliza mbele maslahi ya Taifa kabla ya kitu kingine, akibainisha kuwa sehemu ya uimara wa Taifa uliopo leo umechangiwa na uchapakazi wake mkubwa.
Rais Samia ameyasema hayo wakati wa kuuaga mwili wa Marehemu Jenista Mhagama katika Kanisa Katoliki, Kiwanja cha Ndege, Jijini Dodoma jijini Dodoma, Desemba 13, 2025, ambapo viongozi mbalimbali pamoja na wananchi walikusanyika kumuaga marehemu.
kifo cha Marehemu Jenista Joakim Mhagama kilitokea Desemba 11, 2025, jijini Dodoma,, na mwili wake utapumuzishwa katika nyumba yake ya milele Desemba 16,2025 Katika Kijiji cha Ruanda, Mbinga
Rais Samia amesema Mhe. Jenista Mhagama alipendwa na kuheshimiwa na watu wote hasa waliokuwa chini yake kutokana na utendaji wake uliotukuka, akibainisha kuwa alimpa jina la “kiraka” kwa sababu kila sehemu alipowekwa alikuwa akiitumikia kwa usahihi.
Aidha, Rais Samia, amesema mafanikio ya Bunge na Taifa hutokana na mshikamano wa viongozi wote wakiwemo Wabunge na Mawaziri bila kujali tofauti za aina yoyote, akieleza kuwa Mhe. Jenista Mhagama amefanya kazi kubwa kwa nchi yetu, alikuwa kiongozi jasiri na mlezi wa wengi ndani ya Bunge na Serikali kwa ujumla.
Rais Samia ameongeza kuwa Mhe. Mhagama alikuwa nguzo ya matumaini kwa wanawake na vijana, na alikuwa kiongozi aliyetawaliwa na nidhamu katika utendaji wake.
Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Emmanuel John Nchimbi, amesema kuwa kwa kipindi chote cha uongozi wake, Mhe. Jenista Mhagama alikuwa mtumishi wa kweli, mnyenyekevu na aliwapenda watu wake, akisisitiza kuwa kitu alichotanguliza mbele katika maisha yake ya kazi ni kuwatumikia wananchi wa Peramiho.
Makamu wa Rais amesema kuwa kama Mungu angeniambia aombe kitu kimoja, angeomba Wabunge na Madiwani wote wawapende na kuwatumikia wananchi wao kwa kiwango kama alichofanya Mhe. Jenista Mhagama.
Naye Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mussa Azzan Zungu, ametoa pole kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, familia, Wabunge na Watanzania kwa ujumla kwa kuondokewa na kiongozi mahiri aliyeipenda nchi yake na kazi zake, akisema alikuwa ni mtu aliyejishusha sana kwa wengine.
Awali akizungumza Katibu wa Bunge amesema kuwa aliyekuwa Marehemu Jenista Mhagama, amefariki dunia kutokana na ugonjwa wa moyo, Aidha Katibu wa Bunge amesema marehemu alikuwa akiendelea kupatiwa matibabu kabla ya mauti kumkuta.
Akizungumza kwa niaba ya familia, mtoto wa aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Peramiho, Marehemu Jenista Mhagama, Victor Mhagama, amesema mama yao aliwafundisha kupenda kazi na kuwa na uzalendo kwa nchi yetu, akieleza kuwa aliamini na kuwasihi kumcha Mungu na kuchapa kazi.
Victor amesema marehemu mama yao alijali utu na fadhila, hakujali mkubwa wala mdogo, maskini wala tajiri bali wote aliwasimamia kwa haki na upendo na alikuwa mwana maendeleo.
Pia, amesema kuwa marehemu Jenista Mhagama aliipenda nchi yake na aliwathamini watu wa nchi yake, akisema aliwapenda watu wa Peramiho na aliwafanyia kazi ya dhati.

Picha za matukio mbalimbali wakati wa ibada ya kuaga mwili wa aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Peramiho, Marehemu Jenista Joakim Mhagama katika Kanisa Katoliki Parokia ya Kiwanja cha Ndege, Jimbo Kuu la Dodoma, tarehe 13 Desemba, 2025.
No comments