Breaking News

UJENZI WA DARAJA LA UZI NA BARABARA YA NG’AMBWA WAFIKIA ASILIMIA 70

Na said Khamis.

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhe. Khalid Salum Mohamed, amesema ujenzi wa Daraja la Uzi pamoja na Barabara ya Ng’ambwa, Wilaya ya Kati, unaendelea vizuri ambapo umefikia asilimia 70 ya utekelezaji hadi sasa.

Mhe. Khalid ameyasema hayo wakati wa ziara ya kutembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa daraja hilo lenye urefu wa kilomita 2.2 pamoja na barabara yenye urefu wa kilomita 6.5, ikiwa ni muendelezo wa ziara zake za kukagua miundombinu ya ujenzi. Amesema mradi huo unatarajiwa kuwekewa jiwe la msingi katika sherehe za Maadhimisho ya Mapinduzi mwaka 2026.

Ameeleza kuwa ujenzi wa barabara ya Ng’ambwa umefikia asilimia 55, hali ambayo imewapa faraja wananchi wa kijiji hicho kutokana na kilio chao cha muda mrefu kuhusu ubovu wa miundombinu hiyo.

Aidha, Waziri huyo amesema wananchi waliopitiwa na mradi wameshalipwa fidia, na baadhi yao tayari wameanza kuvunja nyumba zao, huku Serikali ikiendelea na zoezi la kulipa fidia kwa wananchi wengine ili kupisha utekelezaji wa mradi huo.


Akizungumzia ujenzi wa Barabara ya Kitogani-Paje yenye urefu wa kilomita 10, inayotarajiwa kuzinduliwa mwishoni mwa mwezi huu, Mhe. Khalid amesema barabara hiyo imefikia asilimia 80 ya utekelezaji na ni miongoni mwa barabara 277 ambazo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amedhamiria kuzijenga katika maeneo ya mijini na vijijini.

Katika hatua nyingine, Waziri Khalid amewataka madereva kuzingatia alama na ishara za barabarani pamoja na mwendo unaotakiwa, ili kuepusha ajali zisizo za lazima.
Sambamba na hilo amewanasihi wananchi kuzingatia sheria za ujenzi kwa kutojenga katika hifadhi ya barabara, kwa kuacha nafasi ya mita 25 kutoka katikati ya barabara, ili kupisha huduma nyingine muhimu ikiwemo njia za kupitishia maji.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Barabara, Mhandisi Cosmas Masolwa, ameziomba taasisi husika kuharakisha zoezi la kugawa na kupima maeneo ya pembezoni mwa barabara, ili kuzuia ujenzi holela.



Nao wananchi wa kijiji hicho wamesema ujenzi wa daraja na barabara hiyo utaondoa adha waliokuwa wakiipata kwa muda mrefu, hasa kipindi cha mvua kutokana na maji kujaa barabarani na kuwazuia kufanya shughuli zao za kila siku.



No comments