RAIS DKt. HUSSEIN MWINYI AFANYA MABADILIKO YA UONGOZI SERIKALINI
Na Said Khamis.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amefanya uteuzi na uteuzi mpya wa Wakuu wa Mikoa pamoja na Naibu Katibu Wakuu katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kwa lengo la kuimarisha ufanisi wa kiutendaji na usimamizi wa shughuli za Serikali.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Baraza la Mapinduzi, Dkt. Mwinyi amemteua Mhe. Moh’d Ali Abdallah kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi. Kabla ya uteuzi huo, Mhe. Moh’d Ali alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Mjini, Unguja. Aidha, Mhe. Cassian Gallos Nyimbo ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, ambapo kabla ya uteuzi huo alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Kati, Unguja.
Katika mabadiliko hayo ya kiuongozi, Rais Dkt. Mwinyi pia amemteua Mhe. Mgeni Khatib Yahya kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba. Mhe. Mgeni alikuwa akihudumu kama Mkuu wa Wilaya ya Chake Chake, Pemba kabla ya kuaminiwa nafasi hiyo mpya ya uongozi wa mkoa.
Sambamba na uteuzi wa Wakuu wa Mikoa, Rais wa Zanzibar amefanya uteuzi wa Naibu Katibu Wakuu wawili. Ndugu Hawwah Ibrahim Mbaye ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu katika Wizara ya Teknolojia ya Habari, Mawasiliano na Ubunifu, akitokea nafasi ya Naibu Katibu Mkuu (Mawasiliano) katika Wizara iliyokuwa ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi. Vilevile, Dkt. Said Seif Mzee ameteuliwa tena kuwa Naibu Katibu Mkuu katika Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa uteuzi huo umeanza rasmi tarehe 15 Desemba, 2025, na kwamba wateule wote wataapishwa siku ya Jumatano tarehe 17 Desemba, 2025, saa 8:00 mchana katika Ikulu ya Zanzibar.

No comments