RC KUSINI UNGUJA AFANYA ZIARA YA KUSHTUKIZA.
Na Mwandishi wetu .
Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Mhe Hamida Mussa Khamis amewaagiza maafisa utumishi wa Ofisi za Wilaya na Manisapa katika mkoa huo kuhakikisha wanawasilisha ripoti za mahudhurio ya kuingia na kutoka kwa watendaji wa ofisi hizo pamoja na wafanyakazi wa sekta mbali mbali za Serikali wanaofanya kazi zao katika ofisi za wakuu wa Wilaya.
Agizo hilo amelitoa wakati alipofanya ziara ya kushtukiza mapema asubuhi ya leo katika ofisi mbali mbali za tawala za mikoa katika mkoa huo yenye lengo la kuangalia mwenendo mzima wa uingiaji na kutoka pamoja na utoaji wa huduma kwa wananchi wanaofika kupata huduma katika ofisi hizo.
Amesema yapo mapungufu mengi aliyoyabaini kupitia ziara hiyo hivyo amewaagiza Maafisa Utumishi kuandaa ripoti ya kina ya mahudhurio ya wafanyakazi katika taasisi za umma na kuiwasilisha Afisi ya Mkoa muda kila mwisho wa wiki kwani ripoti hizo zitasaidia kubaini hali halisi ya mahudhurio ya wafanyakazi pamoja na changamoto zinazochangia uchelewaji au utoro kazini
Ameeleza kuwa wapo baadhi ya watumishi wa umma wanachelewa kufika kazini na wengine kuondoka mapema jambo ambalo ni kinyume na sheria na taratibu za utumishi wa Umma na linakwamisha upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi wanaofika katika ofizi hizo.
Aidha amefahamisha kuwa maafisa utumishi wamekuwa wakipatiwa mafunzo mbali mbali ya utumishi wa Umma hivyo wanawajibu wa kuhakikisha kuyatuma mafunzo elekezi wanayopewa katika kuwasimamia watendaji kufuata Sheria zinavyoelekeza ili kila mmoja aweze kutimiza majukumu yake aliyopangiwa.
Katika ziara hiyo mkuu huyo wa Mkoa ametembelea Ofisi ya Wilaya Makunduchi, Ofisi ya Baraza la Mji Wilaya ya Kusini, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya Dunga pamoja na Ofisi ya Baraza la Manispaa kati.


No comments