Breaking News



Na Said Khamis.

Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Mheshimiwa Riziki Pembe Juma, amesema ameridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa viwanja vya michezo unaoendelea katika Mkoa wa Kusini Pemba.

Waziri Pembe alisema kuwa miradi yote inaendelea vizuri, licha ya changamoto zilizojitokeza katika ujenzi wa Kiwanja cha Kangani, ambacho kimechelewa kutokana na sababu mbalimbali zinazoikabili.

Ameyasema hayo wakati wa ziara ya kutembelea na kukagua miradi yote ya wizara hiyo kisiwani Pemba, yenye lengo la kujionea maendeleo ya utekelezaji pamoja na kusikiliza changamoto zinazowakabili wakandarasi.

“Miradi inaendelea vizuri, na changamoto zinazojitokeza haziwezi kuepukika, ikiwemo mvua, lakini tumekaa pamoja na wadau na kuweza kuzitafutia ufumbuzi,” alifafanua Waziri Pembe.

Aidha alisema Serikali ya Awamu ya Nane chini ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Hassan Mwinyi, imefanya maboresho makubwa katika miundombinu ya michezo, na kusisitiza kuwa ujenzi huo unapaswa kwenda sambamba na kasi ya Serikali.



Vilevile, aliwashukuru washauri elekezi pamoja na wakandarasi kwa juhudi zao, na kuwataka kuongeza kasi ya ujenzi ili kukabidhi viwanja kwa wakati waliokubaliana.

Katika hatua nyingine, Waziri Pembe alielekeza kuwa ndani ya wiki sita zijazo kujengwe vyoo katika Kiwanja cha Tennis kilichopo Chake Chake Mjini.

Kwa upande wake, Meneja wa Uwanja wa Gombani, Nassir Salim Ali, alisema ujenzi wa uwanja huo umewezesha zaidi ya vijana 500 kupata ajira za muda.

Naye Sheha wa Shehia ya Kichungwani, Yussuf Saleh Salim, aliomba Serikali kujenga uzio wa Kiwanja cha Tennis ili kukilinda dhidi ya uharibifu.

“Kiwanja cha Tennis ni roho ya Mji wa Chake Chake, kwani vijana wengi kutoka maeneo mbalimbali huja kushiriki michezo tofauti, na kimeibua vipaji vingi vya michezo,” alieleza.



Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Skuli ya Msingi Ukutini, Idrisa Khamis Vuai, aliishukuru Serikali kwa juhudi zake za kujenga viwanja vya michezo, akisema vitasaidia watoto na vijana kugundua na kukuza vipaji vyao.


No comments