Breaking News

MADIWANI WATAKIWA KUIMARISHA UTAWALA BORA KUPITIA UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU YAO



Na said Khamis.

Mstahiki Meya wa Jiji la Zanzibar, Kamal Abdulsatar Haji, amewataka Madiwani wa Baraza la Jiji la Zanzibar kuzingatia kikamilifu majukumu, madaraka na mipaka ya uongozi wao ndani ya Serikali za Mitaa ili kuimarisha misingi ya utawala bora.

Meya Kamal ameyasema hayo wakati alipofungua mafunzo maalum kwa Madiwani yaliyofanyika katika ukumbi wa baraza la jiji huko Michenzani, akieleza kuwa mafunzo hayo yameandaliwa mahsusi kwa lengo la kuwajengea uelewa wa kina kuhusu utekelezaji wa majukumu yao kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu.

Amesema Madiwani, kama viongozi wa kuchaguliwa na kuteuliwa, ni kiungo muhimu kati ya Serikali na wananchi, hivyo wanapaswa kusikiliza kero na mahitaji ya wananchi, kuyawasilisha kwenye vikao halali pamoja na kushiriki kikamilifu katika kupanga, kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika maeneo yao.



Vilevile, amewataka Madiwani kuzingatia maadili ya uongozi kwa kuepuka vitendo vya rushwa, upendeleo na matumizi mabaya ya madaraka, akibainisha kuwa wananchi wanawatazama na wanatarajia kuona uongozi unaotanguliza maslahi ya umma kuliko maslahi binafsi.

Meya Kamal ameongeza kuwa mafunzo hayo ni fursa muhimu kwa Madiwani kujifunza mbinu za uongozi shirikishi, utatuzi wa migogoro, usimamizi wa rasilimali za umma pamoja na namna bora ya kushirikiana na wadau wa maendeleo, na amewahimiza kushiriki kikamilifu kwa kuuliza maswali na kuchangia hoja ili kufikia uelewa wa pamoja.

Nae Mkurugenzi wa Baraza la Jiji Salmin Abdallah Amour amesema lengo la mafunzo hayo madiwani wapya ni kuweza kujua kanuni na sheria za baraza la jiji pamoja na kujua wajibu na majukumu yao ya kila siku na madiwani wakongwe kujikumbushia sheria hizo.

Nao madiwani hao wamesema mafunzo hayo yatawasaidia kufanya kazi kwa uweledi na kupelekea kutimiza lengo na adhma ya iliyowekwa na kupelekea kufanya kazi kwa ufanisi wa kazi hizo na kuwataka madiwani wenzao kuyatumia mafunzo waliopewa ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi.



Mafunzo hayo ya siku tatu yanayotolewa katika baraza kwa madiwani wa jiji la zanzibar yatafungwa siku ya jumatano Disemba 24, 2025. 



No comments