Breaking News

Zanzibar yaendelea na maandalizi ya AFCON 2027

 


RAIS wa Zanzibar Dk. Hussein Ali Mwinyi, ametembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa kimkakati wa Zanzibar Sports City unaotekelezwa katika eneo la Fumba, Mkoa wa Mjini Magharibi, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya Michezo ya AFCON 2027.

Katika ziara hiyo, Rais Dk Mwinyi aliihakikishia Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo pamoja na Kampuni ya ORKUN GROUP kuwa serikali imefungua milango kuhakikisha ujenzi huo unafanyika kwa kasi, ufanisi na kwa kuzingatia viwango vya kimataifa.

Aidha, ameitaka Wizara na mkandarasi kutowasilisha changamoto kwa kuchelewa, ili serikali iweze kutoa ufumbuzi wa haraka pale unapohitajika.

Rais Dk. Mwinyi aliambatana na Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Riziki Pemba Juma, pamoja na Naibu Waziri, Ali Abdulgullam Hussein, katika ziara iliyofanyika leo tarehe 18 Novemba 2025.

Uwanja wa mapira katika matengenezo
Mradi wa Zanzibar Sports City ni miongoni mwa miradi ya kimkakati inayotekelezwa na serikali Zanzibar kwa lengo la kuimarisha miundombinu ya michezo na kukuza maendeleo ya sekta hiyo nchini.

Awamu ya kwanza ya mradi huo inajumuisha ujenzi wa uwanja wa kimataifa wa mpira wa miguu wenye uwezo wa kuchukua mashabiki 36,500, pamoja na viwanja viwili vya mazoezi vyenye uwezo wa kuchukua mashabiki 15,000 kila kimoja.

Moja ya viwanja hivyo pia kitatumika kwa ajili ya sherehe za kitaifa. Na kwambamujenzi wa mradi huo unatarajiwa kukamilika ifikapo Disemba 2026.



No comments