DKT. HABIBA ACHUKUA RASMI MAJUKUMU YA UKATIBU MKUU WA BIASHARA NA MAENDELEO YA VIWANDA
Na Kassi Ali.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda, Bi. Fatma Mabrouk Khamis, amekabidhi rasmi Ofisi za Wizara hiyo kwa Katibu Mkuu mpya, Dkt. Habiba Hassan Omar, kufuatia uteuzi wa Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu wa Wizara za SMZ uliofanywa hivi karibuni.
Makabidhiano hayo yamefanyika leo katika Ukumbi wa Wizara ya Biashara uliopo Kinazini, Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja, yakihudhuriwa na watendaji mbalimbali wa wizara hiyo.
Katika uteuzi mpya uliotangazwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Bi. Fatma Mabrouk Khamis amehamishiwa Wizara ya Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu kama Katibu Mkuu mpya wa wizara hiyo.
Akizungumza baada ya makabidhiano, Bi. Fatma aliwashukuru watendaji wote wa Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda kwa mashirikiano yao makubwa katika kutekeleza majukumu ya wizara kipindi chote cha uongozi wake.
Alisema ushirikiano huo umewezesha kufikiwa kwa mafanikio mbalimbali ya kimaendeleo ndani ya wizara, huku akiwataka watendaji hao kuendeleza ari na kasi ya utendaji ili kuunga mkono malengo ya Serikali ya Awamu ya Nane.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu mpya, Dkt. Habiba Hassan Omar, aliwaasa watendaji wa wizara kuhakikisha wanadumisha nidhamu, weledi na ushirikiano wa karibu katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.
Dkt. Habiba alibainisha kuwa utekelezaji wa majukumu kwa ufanisi ndiyo nguzo kuu ya kufanikisha malengo makuu ya wizara, ikiwemo kuchangia kwa kasi ukuaji wa uchumi kupitia sekta ya biashara na viwanda.
Aidha, aliwataka watendaji kuwa wabunifu na kufuata maelekezo ya serikali kwa wa.kati, akisisitiza kuwa wizara hiyo ina wajibu mkubwa katika kuimarisha mazingira wezeshi ya biashara kwa maslahi ya wananchi wa Zanzibar.
Makabidhiano hayo yamefanyika leo katika Ukumbi wa Wizara ya Biashara, Kinazini, Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja
Reviewed by ZANNEWS UPDATE
on
November 26, 2025
Rating: 5



No comments