Breaking News

WADAU WA SERIKALI WATAKIWA KUONGEZA UBUNIFU KUKABILIANA NA USAFIRISHAJI HARAMU WA BINADAMU.



Na Siti Ali.

Taasisi zinazohusika na kuzuia na kupambana na usafirishaji haramu wa binaadamu zimetakiwa kutumia ubunifu mkubwa katika kubaini vyanzo na mitandao inayohusika na uhalifu huo, ili kukomesha vitendo vinavyoathiri kwa kiasi kikubwa wanawake na watoto nchini.

Wito huo umetolewa leo Novemba 26, 2025 katika Kikao cha Wadau wa Serikali kilichofanyika Mwembe Madema, Mkoa wa Mjini Magharibi, Zanzibar, kwa lengo la kuimarisha ushirikiano katika kuzuia na kupambana na uhalifu wa usafirishaji haramu wa binadamu.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao hicho, Mkurugenzi wa Uratibu wa Shughuli za Serikali kutoka Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Siajabu Suleiman Pandu, alisema kukithiri kwa matukio ya usafirishaji haramu kunahitaji ubunifu na mikakati mipya ili kufichua mitandao inayojihusisha na vitendo hivyo.

Alisema jamii inapaswa kushiriki kikamilifu kwa kutoa taarifa za viashiria au matukio kwa mamlaka husika ili hatua madhubuti ziweze kuchukuliwa kwa wakati na kuzuia madhara zaidi.

Kwa upande wake, Afisa Mwandamizi wa Sekretarieti ya Kuzuia na Kupambana na Usafirishaji Haramu wa Binaadamu, Rafii Said Mnete, alisema Serikali kupitia sekretarieti hiyo imeandaa mpango wa kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha udhibiti na kupambana na uhalifu huo katika maeneo mbalimbali nchini.

Alisema hatua hizo zinajumuisha kutoa elimu kwa jamii, kuimarisha uchunguzi, kushirikiana na taasisi za kimataifa, pamoja na kutumia mifumo ya kisasa katika kufuatilia mienendo ya kihalifu.

Naye Naibu Katibu wa Sekretarieti hiyo Kanda ya Zanzibar, Huzaimat Bakar Kheir, alisema kikao hicho kimekusudia kuzileta taasisi mbalimbali pamoja ili kuongeza ushirikiano na kupanga mikakati shirikishi ya kukabiliana na usafirishaji haramu wa binadamu.



Huzaimat alibainisha kuwa ushirikiano wa karibu baina ya wadau wa serikali na jamii ndio msingi wa kufanikisha mapambano dhidi ya uhalifu huu unaotishia usalama wa raia, hasa makundi yaliyo katika mazingira hatarishi.

Aidha, wadau waliohudhuria kikao hicho walitoa mapendekezo mbalimbali, ikiwemo kuimarisha mafunzo kwa maafisa wanaohusika na utekelezaji wa sheria, kuboresha mifumo ya utoaji taarifa, na kufanya uchambuzi wa kina wa sababu zinazopelekea watu kuingia katika vitendo vya kusafirishwa kiharamu.

Kikao hicho pia kilisisitiza umuhimu wa kufanya kampeni endelevu za uhamasishaji ili kuhakikisha jamii inatambua madhara ya usafirishaji haramu wa binadamu na kuchukua hatua za kuzuia kabla ya madhara kutokea.




No comments