Breaking News

SARATANI YA MATITI BADO NI TATIZO KWA WANAWAKE NA WASICHANA DUNIANI.



Na Siti Ali.

Saratani ya matiti ndiyo inayoongoza duniani ambayo ni chanzo kikuu cha vifo vinavyohusiana na saratani kwa wanawake.

Utambuzi wa mapema ni muhimu sana ili kupata  matokeo mazuri  na kuongeza uwezekano wa kupona. Katika mwezi wa Oktoba, ambao duniani kote unatambuliwa kama mwezi wa uhamasishaji dhidi ya saratani ya matiti, Shirika la Afya Duniani (WHO) linaelekeza juhudi zake katika kuongeza uelewa, kuhimiza uchunguzi wa mapema, na kuimarisha huduma za matibabu na kinga. Kwa mujibu wa takwimu za kimataifa, inakadiriwa kuwa kila baada ya dakika nne, mwanamke hugunduliwa na saratani ya matiti, jambo linaloonesha uzito wa tatizo hili kiafya na kijamii.

Licha ya kuongezeka kwa ugonjwa wa saratani ya matiti kwa wanawake, zipo jitihada mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali pamoja na wadau ili kupunguza kasi ya maambukizi na athari zake. Jitihada hizo zinajumuisha utoaji wa elimu kuhusu ugonjwa huo, ikiwemo namna ya kujichunguza mwenyewe hatua ambayo inawasaidia wanawake wengi nchini kutambua dalili za awali.

Akizungumzia juhudi hizo, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Jamii kutoka Asasi ya Jafaygo, Dkt. Merry Rose Kawajiata, alisema kuwa wamekuwa wakishirikiana na Wizara ya Afya chini ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kutoa mafunzo kwa wahudumu wa afya ili kuwawezesha kufanya uchunguzi wa saratani ya matiti kwa ufanisi.

“Tumekuwa tukishirikiana na Wizara ya Afya kupitia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kutoa mafunzo kwa wahudumu wa afya ili waweze kufanya uchunguzi wa saratani ya matiti, pamoja na kutoa matibabu ya awali mara tu ugonjwa huu unapogundulika,” alieleza Dkt. Merry.

Hata hivyo, Dkt. Merry alisema kuwa zaidi ya asilimia 50 ya wanawake hupoteza maisha kutokana na saratani ya matiti, sambamba na kueleza viashiria vinavyochangia kupatikana kwa ugonjwa huo, ikiwemo umri, urithi, uzito mkubwa, kutokunyonyesha, kutofanya mazoezi, matumizi ya tumbaku, na kuchelewa kupata mtoto.



“Hakuna sababu moja maalumu inayosababisha saratani ya matiti, bali vichocheo vya hatari vinavyoweza kuchangia ni pamoja na kupata hedhi mapema kabla ya umri wa miaka 11, kuchelewa kukoma hedhi zaidi ya miaka 55, kuwa na historia ya saratani katika familia au kupata saratani kwa njia ya kurithi. Aidha, wanawake kutokunyonyesha au kunyonyesha kwa muda mfupi, kuwa na uzito mkubwa kupita kiasi, kupata mtoto baada ya miaka 35, pamoja na matumizi ya tumbaku au pombe, ni miongoni mwa sababu zinazoongeza hatari,” alifafanua Dkt. Merry.

Kwa upande wake, Afisa wa Maradhi ya Saratani ya Matiti na Mlango wa Kizazi kutoka Wizara ya Afya, Kitengo Shirikishi cha Mama na Mtoto, Mwanafatima Ali Mohammed, kwa ushirikiano na Asasi ya Jafaygo kupitia ufadhili wa Faidha Foundation, alisema wamekuwa wakitekeleza jitihada mbalimbali za utoaji elimu kwa jamii kwa kutembelea wilaya na shehia mbali mbali ili kuwafikia wanawake wengi zaidi kwa ajili ya elimu na uchunguzi wa saratani ya matiti.

 

Alisema kuwa takwimu za mwaka jana zinaonesha kuwa mwezi Juni pekee, watu 7,400 waliweza kufanyiwa uchunguzi wa saratani ya matiti Unguja na Pemba. Aidha, kuanzia Juni hadi Oktoba mwaka huu, watu wasiopungua 3,000 tayari wamepimwa, na zoezi hilo linaendelea.

Mwanafatima alitoa wito kwa jamii kuendelea kujenga utamaduni wa kutembelea vituo vya afya kwa ajili ya kujichunguza, akisisitiza kuwa saratani ya matiti ikigundulika mapema inatibika.

Subira Ali Hamza, mama wa watoto watatu kutoka Matemwe na mmoja wa waliowahi kuathirika na saratani ya matiti, alielezea namna alivyogundua ugonjwa huo na kupatiwa matibabu hadi kupona, huku akitoa shukurani kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Kitengo Shirikishi cha Mama na Mtoto kwa huduma alizopata.

“Mimi nilianza kuhisi maumivu ya ziwa nikaanza kutumia dawa za kienyeji, lakini siku moja nikasikia gari la matangazo likitoa elimu kuhusu saratani ya matiti. Niliamua kuchukua hatua na kufika hospitali, ambako nilipatiwa matibabu na kwa neema ya Mungu niliweza kupona na sasa afya yangu imeimarika,” alisema Subira.

Alitoa wito kwa wanawake na wasichana kutokukimbilia tiba zisizothibitishwa na badala yake kufika hospitali mapema pindi wanapohisi mabadiliko yoyote, ili kupata uchunguzi na matibabu sahihi.

jamii imesisitizwa kuchukua tahadhari kwa kujenga utamaduni wa kuchunguza afya mara kwa mara, kuachana na mila potofu zinazoathiri juhudi za matibabu, na kuhakikisha wanawahi kupata huduma za hospitali kwa kuwa saratani ya matiti inatibika ikiwa itagundulika mapema. Kinga ni bora kuliko tiba.


No comments