UUZAJI HOLELA WA POMBE WATIKISA MAADILI YA VIJANA BUNGI MCHANGANI, SERIKALI YAOMBWA KUINGILIA KATI.
Na Said Khamis Wilaya ya Kati, 27/11/2025
Uwepo wa nyumba za kuuzia vileo katika mitaa ya Shehia ya Bungi Mchangani umeibua malalamiko kutoka kwa wananchi ambao wanasema biashara hiyo imesababisha kuporomoka kwa maadili kwa baadhi ya vijana na hata watoto.
Wakizungumza na TOZ, wananchi wamesema baa hizo za mitaani zimekuwa kichocheo cha vitendo viovu ikiwemo ulevi uliopitiliza, wizi wa mazao na mifugo pamoja na ongezeko la vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia kwa wanawake na watoto.
“Vijana wetu wadogo wanajiingiza kwenye ulevi kupita kiasi, wengine wanaiba mazao na mifugo. Hali hii inatuumiza sisi kama wazazi,” walisema baadhi ya wananchi.
Mbali na uuzaji holela wa pombe, wananchi pia wamelalamikia ubigaji wa miziki usiofuata sheria na unaochafua mazingira ya makazi yao.
Kwa upande wake, Mjumbe wa Sheha wa shehia hiyo, Bi. Dawa Hussein Makame, amesema uongozi wa shehia umeshachukua hatua za awali kushughulikia changamoto hiyo kwa kushirikiana na wananchi.
“Mimi na sheha tumekaa pamoja kujadili namna ya kuondoa baa hizi za mitaani na kuwachukulia hatua wale wanaokaidi sheria,” alisema Bi. Dawa.
Amesema tayari malalamiko ya wananchi yamefikishwa katika mamlaka husika ili kufanyika kwa uchunguzi na kuchukua hatua kwa wamiliki wa baa hizo na wauzaji pombe wanaokiuka sheria.
Naye Katibu wa Kamati ya Maadili wa Jumuiya ya Maimamu Zanzibar (JUMAZA), Sheikh Abdallah Mnubi Abasi, ameikumbusha serikali kusimamia ipasavyo Sheria Namba 9 ya Vileo ambayo inaelekeza baa kuwa mbali na makazi ya watu.
“Endapo serikali itasimamia kikamilifu sheria zilizopo, tutapunguza utitiri wa baa katika maeneo ya makazi,” alisema Sheikh Mnubi.
Ameongeza kuwa JUMAZA tayari imeanza kuchukua jitihada mbalimbali ikiwemo kuhamasisha masheha na kutoa elimu kwa wananchi ili kuhakikisha changamoto hiyo inapungua na hatimaye kuisha kabisa.

.jpeg)
.jpeg)
No comments