Breaking News

Simba yaanika mkakati kuifuata Stade Malien

 


KIKOSI cha Simba kimerejea mazoezini jana baada ya kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Atletico Petroleos de Luanda, kikitarajia kuondoka kesho alfajiri kuelekea nchini Mali kwa ajili ya mchezo wa pili, Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Stade Malien, huku viongozi wa klabu hiyo wakiwatuliza wanachama na mashabiki wake.

Meneja Habari na Mawasiliano wa Klabu hiyo, Ahmed Ally, alisema jana, baada ya mchezo wa Jumapili kuwa, wachezaji walipata mapumziko ya siku moja, ambapo jana walirejea mazoezini kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wa pili wa Kundi D, dhidi ya Stade Malien ya Mali, Jumapili wiki hii.

"Baada ya mchezo tuliwapa wachezaji mapuziko wa siku moja, (leo) jana, wamerejea mazoezini, kikosi chetu kinatarajiwa kuondoka Alhamisi alfajiri kuelekea nchini Mali kupitia Addis Ababa nchini Ethiopia, tunakwenda tukiwa na kumbukumbu ya kupoteza mchezo wa kwanza nyumbani, hivyo hatutokubali hilo litokee tena," alisema Ahmed.

Aliwataka wanachama na mashabiki wa Simba kutulia hasa baada ya matokeo hayo, akisema huu si wakati wa kuvurugana, bali wa kuwa wamoja ili kufanya vema katika michezo ijayo.

"Wanasimba wenzangu hatupaswi kuvurugana, wala kukataa tamaa, bado tuna nafasi kubwa ya kufanya vizuri katika mechi zijazo. Muhimu ni kurejea katika uwanja wa mazoezi kurekebisha tulipokosea na kurejea kwa nguvu kubwa katika uwanja wa mapambano. Tusijitoe wenyewe kwenye mashindano, tuzungumze yote, lakini tusisahau kuwatia moyo wachezaji na kuwapa nguvu watupambanie mechi zijazo," alisema na kuongeza.

"Imani yangu, Simba hasa kimataifa haijawahi kuyumba, haijalishi tumeanzaje au tumepoteza mara ngapi, lakini daima mwisho wetu huwa ni mzuri."

Wanachama na mashabiki wa timu hiyo wameonekana kuwa na wasiwasi na kikosi hicho ambacho hakijashinda mchezo wowote wa Ligi ya Mabingwa msimu huu kikiwa nyumbani, Uwanja wa Benjamin Mkapa, ambao wao wanaufahamu kuwa ni 'machinjio' ya timu za kigeni kila zinapokuja hapo.

Kabla ya kuchapwa bao 1-0 Jumapili iliyopita dhidi ya Waangola hao, ilicheza michezo mingine miwili bila kupata ushindi iliotoka sare bao 1-1, Septemba 26, mwaka huu, dhidi ya Gaborone United, katika mchezo wa marudiano ya hatua za awali Ligi ya Mabingwa, lakini ilitinga raundi ya kwanza baada ya kushinda ugenini bao 1-0.

Oktoba 26, mwaka huu ililazimishwa suluhu dhidi ya Nsingizini Hotspur, lakini iliingia hatua ya makundi ikinufaika na ushindi wa mabao 3-0 iliyoupata ugenini.

Simba ilipoteza mechi yake Jumapili iliyopita kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kwa mara ya kwanza, baada ya miaka miwili.

Mara ya mwisho ilikuwa ni Februari 18, 2023, ilipochapwa mabao 3-0 dhidi ya Raja Casablanca ya Morocco.



No comments