WAZIRI PEMBE ATAKA MAAGIZO YA RAIS MWINYI YATEKELEZWE KWA UMAKINI.
NA ASYA HASSAN 25/11/2025.
WAZIRI wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Riziki Pembe Juma, amewataka watendaji wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kufuata kwa umakini maelekezo ya Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, akisema ndiyo msingi wa kufanikisha malengo ya wizara.
Waziri Pembe alitoa kauli hiyo wakati wa hafla ya makabidhiano ya ofisi iliyofanyika katika Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Kinazini, hafla iliyowakutanisha watendaji na viongozi wapya wa wizara hiyo.
Alisema Rais Mwinyi amesisitiza mambo kadhaa muhimu, likiwemo utekelezaji wa ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), kufanya kazi kwa pamoja kama timu, na kusimamia kwa ukaribu dira ya maendeleo ya serikali.
Alisema maelekezo ya Rais si ya kupuuzwa, bali ni dira ya kuongoza utendaji wa kila siku katika wizara zote, hususan zinazogusa moja kwa moja ustawi wa wananchi.
Waziri Pembe alisema kuwa utekelezaji sahihi wa ilani ya CCM ndiyo msingi wa kuhakikisha huduma zinazotolewa zinamgusa moja kwa moja mwananchi.
Aliongeza kuwa bila ushirikiano wa timu (teamwork) na uwajibikaji wa pamoja, wizara haiwezi kufanikisha majukumu yake ipasavyo.
“Ni muhimu kufanya kazi kwa umoja, kwa nidhamu na kwa kujituma, hicho ndicho Rais anakitaka, na ndicho kinachohitajika ili twende sambamba na mwelekeo wa maendeleo ya nchi,” alisema Waziri Pembe.
Mbali na hayo, Waziri huyo aliwahimiza watendaji kujenga utamaduni wa kupeana taarifa, kujadiliana na kutatua changamoto kwa pamoja ili kuongeza ufanisi wa wizara.
Aidha, aliwashukuru watumishi wa wizara hiyo kwa ushirikiano waliompa wakati wote alipokuwa akiongoza wizara hiyo kabla ya mabadiliko.
Aliwataka waendelee kuwapa viongozi wapya ushirikiano huo huo ili kuhakikisha malengo ya wizara yanatekelezwa bila vikwazo.
Kwa upande wake, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Anna Athanas Paul, aliwataka watendaji wa wizara hiyo kumpa ushirikiano wa kutosha katika kutekeleza majukumu yake.
Waziri Anna alisema yupo tayari kufanya kazi kwa karibu na wafanyakazi wote ili kuendeleza maendeleo ndani ya wizara hiyo.
Alisema milango yake ipo wazi kwa ushauri, maoni na mapendekezo yoyote yatakayosaidia kuboresha huduma zinazotolewa na wizara hiyo.
“Nataka tushirikiane kwa dhati kusimamia ilani ya CCM na dira ya serikali, ili kuhakikisha tunawafikia wananchi kwa huduma bora na zenye ufanisi,” alisema Waziri Anna.
Aliongeza kuwa dhamira yake ni kuona wizara hiyo inakuwa mstari wa mbele katika kulinda haki na ustawi wa makundi mbalimbali katika jamii.
Naye Naibu Waziri wa wizara hiyo, Zawadi Amour Nassor, aliwataka watumishi kuendelea kuwa waadilifu na kujituma katika majukumu yao.
Alisema wizara hiyo inabeba dhamana kubwa ya kusimamia masuala nyeti yanayohusu jamii, jinsia na ustawi wa watoto, hivyo inahitaji mshikamano na uwajibikaji wa dhati.
Hivyo aliwataka watendaji kuimarisha ushirikiano na kuhakikisha kila mmoja anatimiza wajibu wake ili kufanikisha mikakati ya serikali.
Alisisitiza kuwa uwajibikaji wa pamoja ndio utakaowezesha wizara kuleta maendeleo kwa jamii kwa ufanisi na kwa wakati.
No comments