WASHIRIKA WA MAENDELEO WAZINDUA MPANGO WA PAMOJA KUINUA UCHUMI NA KUJENGA JAMII SALAMA ZANZIBAR
Washirika wa maendeleo kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na asasi za kiraia wamezindua rasmi mpango wa pamoja unaolenga kuinua uchumi wa wananchi na kujenga jamii salama, katika visiwa vya Unguja na Pemba.
Ziara ya siku mbili iliyofanyika mkoa wa Kaskazini Unguja imetoa nafasi ya kuwatambulisha wananchi mradi huo wa mwaka mmoja, unaotekelezwa na mashirika ya UN Women, UNDP, UNFPA, FAWE na TAMWA Zanzibar, kwa kushirikiana na Serikali, ambao utatekelezwa Kaskazini Unguja na Kaskazini Pemba.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Wanawake (UN Women), Bi. Lucy Tesha, alisema mpango huo unalenga kuwawezesha wananchi, hususan wakulima wa mazao ya kiuchumi, kuongeza thamani ya bidhaa zao na kupata masoko yenye tija.
“Lengo letu ni kukuza kipato cha wananchi kupitia shughuli za kiuchumi ikiwemo kilimo cha mazao mbalimbali, sambamba na kuhakikisha wanakingwa dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia katika mnyororo mzima wa thamani. Pia tunatoa uelewa namna ya kupambana na ukatili na udhalilishaji wa kijinsia katika jamii,” alisema Bi. Tesha.
Kwa upande wake, Afisa Ustawi wa Jamii Wilaya ya Kaskazini ‘B’, Mmanga Machano, alisisitiza haja ya kufanya juhudi za ujumuishi wa kijinsia ili elimu na fursa zitolewe kwa wananchi wengi zaidi, jambo litakalowawezesha wanawake kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi.
kwa upande wao wananchi waliokutana na washirika wa maendeleo kupitia vikundi vya kilimo walibainisha changamoto wanazokabiliana nazo ikiwemo kubezwa kwa maneno ya kejeli, kukatishwa tamaa, kunyimwa ruhusa ya kufanya kazi kwa uhuru, pamoja na udhalilishaji kwenye masoko.
Mradi huu unatarajiwa kuwa chachu ya kupunguza umasikini na kuimarisha ulinzi wa jamii dhidi ya ukatili wa kijinsia, huku ukilenga kujenga mazingira salama na jumuishi kwa wananchi wote wa Zanzibar

No comments