Breaking News

Wadau wa Mazingira Pemba Watoa Wito wa Ushirikiano Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabia Nchi.

 


Na mwandishi wetu Pemba. 24/11/2025.

 Jamii kisiwani Pemba imetakiwa kuongeza juhudi za pamoja katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, hali ambayo inaendelea kuathiri shughuli mbalimbali za kibinadamu ikiwemo kilimo, uvuvi na miundombinu. 

Wito huo umetolewa katika mkutano wa wadau wa mazingira uliofanyika katika Ukumbi wa Manispaa ya Chake Chake, Mkoa wa Kusini Pemba.

Akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Mwavuli wa Asasi za Kiraia Zanzibar, Hassan Khamis Juma, alisema mabadiliko ya tabia nchi ni changamoto mtambuka inayogusa maeneo mengi, yakiwemo bahari na ardhi. Alisema ili kukabiliana na athari zake, kunahitajika mashirikiano ya pamoja kati ya serikali, taasisi binafsi na jamii kwa ujumla.

Aidha, alibainisha kuwa uharibifu wa mazingira umeendelea kuchangia kwa kiwango kikubwa kasi ya mabadiliko hayo, hivyo hatua madhubuti zinapaswa kuchukuliwa ili kupunguza athari zinazojitokeza siku hadi siku.



Kwa kutoa ufafanuzi kuhusu umuhimu wa kutunza mazingira, Dkt. Salim Hamad Bakar kutoka Idara ya Mazingira Zanzibar, alisema ni wajibu wa kila mwananchi kuhakikisha anachukua hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi ili kulinda usalama wa vizazi vya sasa na vijavyo. Alisisitiza kuwa matumizi bora ya ardhi, utunzaji wa vyanzo vya maji na kupunguza ukataji wa miti ni miongoni mwa hatua muhimu zinazopaswa kuzingatiwa.

Naye Afisa kutoka Ofisi ya Mratibu wa Asasi za Kiraia, Sada Abubakar Khamis, alieleza kuwa elimu kuhusu hifadhi ya mazingira inapaswa kuendelea kutolewa kwa jamii ili kuongeza uelewa na ushiriki wa wananchi katika mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi.

Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo walieleza kuwa kuongeza upandaji wa miti, kuimarisha usafi wa mazingira na kupunguza matumizi ya plastiki ni miongoni mwa njia bora zitakazosaidia kupunguza madhara ya mabadiliko ya tabia nchi. Walisema kuwa bila ushirikiano wa makundi yote, juhudi za kukabiliana na changamoto hiyo zitakuwa ngumu kufanikiwa.



Mkutano huo uliwaleta pamoja wadau kutoka taasisi mbalimbali za serikali, asasi za kiraia na wanajamii kwa lengo la kuimarisha mikakati ya pamoja ya kulinda mazingira ya Zanzibar.



No comments