Breaking News

UWELEWA MDOGO JUU YA SARATANI YA MATITI BADO NI KIKWAZO KWA ZANZIBAR.


Na Siti Ali

Licha ya serekali kusherekea siku ya wanawake duniani kila mwaka , lakini  yapo matatizo mbali mbali ambayo yanawakabili wanawake ikiwemo saratani ya matiti hali ambayo inawasumbua wanawake wengi wa duniani.

Saratani ni aina ya ugonjwa unaosababishwa na ukuaji wa seli za mwili kubadilika na kukua bila mpangilio maalum.

Saratani ya matiti hutokea kwenye titi ambalo kwa kawaida lina sehemu ya kutengeneza maziwa ijulikanayo kama lobules na aina fulani ya mishipa inayounganisha hizi lobules na chuchu za titi.

 Sehemu kubwa iliyobakia ya matiti inajumuisha mafuta na tishu ambazo kitaalamu zinazoitwa connective and lymphatic tissue. Saratani ya matiti inayotokea kwenye lobules huitwa lobular carcinoma na ile inayotokea kwenye ducts huitwa ductal carcinoma.

Baadhi ya saratani ya matiti zinaongeza ukubwa kutokana na kuwa na vishikizi aina ya receptors zinazojulikana kama estrogen receptors kwenye seli zao ambazo husababisha ukuaji wa saratani ya matiti.

Ili kuimarisha vyema afya ya wananchi kitengo kishirikishi cha afya ya uzazi, mtoto, kijana na lishe mbali ya kuratibu masuala ya afya ya uzazi kwa mama na mtoto lakini pia kinatoa uchunguzi wa saratani ya matiti kwa kinamama kwa kushirikiana na wataalamu wengine.

Huduma hizo za uchunguzi wa awali hutolewa katika hospitali za dispensari hadi hospitali za wilaya, kwani jitihada za kitengo hichi zimewezesha kuokoa maisha ya wanawake na wasichana hapa nchini.

Wataalamu wanaeleza kwamba maradhi ya saratani ya matiti yamekuwa ni chanzo cha vifo kwa kinamama na wasichana wengi ulimwenguni kote.

Ifahamike kuwa ugonjwa huu wa saratani ya matiti unatokana na mabadiliko ya chembe chembe hai katika matiti ambazo hugawanyika na kukua bila ya kidhibiti cha kawaida,ambao unaathiri watu wengi katika jamii,ambapo Tanzania ugonjwa huu unazidi kungezeka kila uchao .

Kwa mwaka 2023 Tanzania imekadiriwa kuwa na wagojwa wapya wa saratani wapatao takribani elfu 42 kwa mwaka takwimu hizi ni kwa wale wanaofika vituo vya afya kwa kufuata matibabu.

Taasisi ya saratani ya Ocian Road imehudumia idadi ya wagonjwa 1141 ambao waligundulika na saratani ya matiti kwa mwaka 2022-2023.Kwa Zanzibar wagonjwa waliogundulika ni asilimia 18 tu kwa mwaka 2021,2022 na 2023,ambapo kwa mujibu wa takwimu hizo zinaonesha kwamba saratani ya matiti bado ni tatizo.

Msaidizi meneja katika kitengo cha maradhi yasiyoambukiza kutoka hospitali ya Mnazi Mmoja Daktari Zuhura Swaleh Amour amesema kuwa Zanzibar uwelewa bado ni mdogo kwa wanajamii kuhusu ugonjwa wa saratani ya matiti kwani ugonjwa huu husababisha vifo vingi  pamoja na ulemavu hutokea juu ya ugonjwa.

Ingawa hakuna sababu maalumu inayosababisha ugonjwa huu isipokuwa vipo viashiria vinavyosababisha saratani ya matiti kama vile umri,urithi,uzito mkubwa ,kutokunyonyesha,kutokufanya mazoezi, matumizi ya tumbaku,kutokuzaa kwa muda mrefu.

“Sababu au vichocheo vinavyochangia kupata saratani ya matiti ni pamoja na kupata hedhi mapema chini ya umri wa miaka 11  na kuchelewa kukoma hedhi zaidi ya miaka 55,kuwepo kwa historia ya saratani katika familia ama kupata saratani kwa njia ya kurithi ,pia ni miongoni mwa sababu za kupata saratani.

Akinamama kutokunyonyesha au kunyonyesha kwa muda mfupi pia ni kichocheo cha saratani ya matiti , au kuwa na uzito mkubwa wa kupitiliza,kuchelewa kupata mtoto zaidi ya miaka 35 sambamba na kujikita katika matumizi ya  tumbaku au pombe”anaeleza daktari Zuhura.

Sehemu ya titi la mama imetajwa kuwa ni yenye kuathirika pia na saratani ya matiti ambapo miongoni mwa dalili zake nikuwasha ,kuchubuka,na sehemu ya titi kubonyea ndani ,kutoka majimaji damu na usaha na maumivu muda wote.

Katibu wa taasisi ya kijamii inayosaidia wananchi Zanzibar (ZOP)Daktari Naufal Kassim Mohammed anaelezea dalili na ishara za saratani ya matiti na kusema kuwa  zinatafautiana kati ya mwanamke na mwanamke ambapo dalili moja wapo au zaidi zinaweza kujitokeza kwa mwanamke aliyepata saratani ya matiti ikiwa ni pamoja na kuhisi  uvimbe au fundo gumu linalofanana na mbegu ndani ya titi au kwapani ,kuwa na uvimbe, ngozi kugeuka rangi.

Dalili nyengine kuwa na ujoto ,kupiga rangi nyekundu au weusi kwenye titi na kubadilika kwa ukubwa au umbo halisi la titi,dalili nyengine ni ngozi kujikunja au kuwa na vijitundu na kuifanya iwe kama ganda la chungwa.

“Dalili ya awali inayoweza kutambulisha saratani ya matiti ni kuwepo kwa uvimbe kwenye titi ambao huwa na hali tofauti na sehemu nyingine za titi. Hata hivyo, si kila uvimbe kwenye titi unaashiria uwepo wa saratani ya matiti. Uvimbe huu huwa mgumu, unaochezacheza kwenye titi, ambapo wakati mwingine unaweza kuwa na maumivu makali au kusiwe na maumivu yeyote. Uvimbe huu huwepo zaidi ya mzunguko mmoja wa hedhi kwa wale ambao hawajaacha kupata hedhi”Daktari Naufal anaeleza.

Wahenga walisema kama huna ushahidi wa jambo huna haki ya kusema jambo kama anavyoeleza Bimwanakhamis Muhammed Abdallah ambae ni muhanga wa maradhi saratani ya matiti amesema kuwa saratani ipo na inaendelea kuondoa uhai wa wanawake na wasichana pamoja na kusababisha ulemavu kwani alijigundua kuwa na ugonjwa huo na kupatiwa matibabu na badala yake akapona .

“Mimi nilijiona na boje katika ziwa langu la kushoto tangu 2007 ndipo nikaenda hospitali kufanya uchunguzi na vipimo na nikagundulika nna saratani ya titi ndipo nikapatiwa matibabu ambayo nimepona hadi leo kwani saratani ya matiti inatibika ukiiwahi mapema na mimi nimepona namshukuru Mungu”anaeleza Bimwanakhamisi.

Aidha Bimwanakhamis ametoa wito kwa jamii kuwa na tabia ya kujichuza matiti yao mara tu baada ya kumaliza mzunguko wa mwezi kwa wale wanaopata hedhi pamoja na kuuona na daktari ili kupata elimu ya kujichunguza wenyewe pindi wanapokuwa majumbani.

“Wito wangu kwa jamii  kuwa na tabia ya kujichuza matiti yao mara tu baada ya kumaliza mzunguko wa mwezi kwa wale wanaopata hedhi pamoja na kuonana  na daktari ili kupata elimu ya kujichunguza wenyewe pindi wanapokuwa majumbani”anasema Bimwanakhamis.

 


Sheha wa Shehiya ya Kikwajuni Juu Asha Ali Ali amekiri kuwepo kwa maradhi ya saratani ya matiti ambayo inawaathiri wanawake na wasichana ulimwenguni kote na kuitaka jamii kuwa na tabia ya kwenda hospitali mara kwa mara kuchunguza afya zao pamoja na kupata elimu juu ya kujichunguza maradhi haya.

“Maradhi ya saratani ya matiti yapo na yanaathiri wanawake wengi na wasichana ulimwenguni kwani husababisha kifo au ulemavu wa kudumu,hivyo natoa wito kwa jamii kujenga tabia ya kukwenda hospitali mara kwa mara ili kupata hupata huduma za afya ikiwemo elimu ya kujichunguza mwenyewe saratani ya matiti”anaeleza Biasha.

Ili kujiepusha na maradhi haya jamii inapaswa kuchukuwa tahadhari ya kujikinga na ugonjwa huu wa saratani ya matiti ikiwa ni pamoja na kufahamu hali ya kawaida ya matiti kwa kujitizama kwenye kioo au kujigusa, kubadili mtindo wa maisha ikiwa ni pamoja na kuzingatia kuwa na uzito kulingana na ushauri wa wataalamu wa afya ,kufanya mazoezi mara kwa mara ni muhimu sana kwa maendeleo mazuri ya afya.

Pia jamii inaaswa kuepuka unywaji wa pombe na matumizi ya tumbaku na uvutaji wa sigara,kila mmoja ahakikishe anatumia matunda na mboga mboga kila siku na kuepuka kula vyakula vya makopo na visivyo vya asili.

Kwa upande wa kinamama wanatakiwa kunyonyesha kwa kuzingatia ushauri wa wataalamu wa afya

 Wizara ya afya inatakiwa izidi kutoa huduma ya saratani kupitia hospitali zake pamoja na vitengo vyake vya afya ya uzazi mama na mtoto  vijana na lishe kupitia wadau mbali mbali wa maendeleo na kuzidisha mashirikiano makubwa kwa wataalamu na madaktari bingwa wa kada hizo.

Kinga ni bora kuliko tiba watu wote wanapaswa kuchukuwa tahadhari kabla ya athari, kama una saratani ya matiti au dalili nyengine usisite kwenda kituo cha afya kwa ushauri na uchunguzi zaidi, kata ukimya kwa kuzungumza na familia yako ili ujue kuhusu historia ya afya katika familia yako.

Jenga utamaduni wa kuzungumza na daktari kuhusu afya yako ya kupata saratani ya matiti na zungumza na daktari ili ujue wakati bora wa kufanya uchunguzi wa kitabibu wa matiti, inawezekana saratani ya matiti ukiiwahi mapema inatibika, kila mtu atimize wajibu wake.


No comments