Breaking News

TAUSI YATOA FILAMU YA UHAMASISHAJI JAMII KUHUSU UTUNZAJI WA MACHO

 


NA Siti Ali.

Kikundi cha Sanaa ya muziki ya tarabu asilia Zanzibar (TAUSI) kimesema kitaendelea kushirikiana na Serekali katika  kutoa elimu juu ya matatizo ya macho ili kuepusha ulemavu unaoweza kutokea.

Akizungumza mara baada ya uzinduzi wa filamu inayohusu umuhimu wa macho huko katika ukumbi wa sheikh Idrisa Abdul Wakili, Mwenyekiti wa kikundi hicho Bimaryam Hamdani amesema kuwa lengo la filamu hiyo ni kuihamasisha jamii umuhimu wa kuyatunza macho ambayo ni kiungo muhimu katika mwili wa binaadamu.

Aidha amesema walemavu wa macho wanapitia changamoto mbali mbali ikiwemo kukosa mashirikiano kwa baadhi ya wanajamii hususani katika masuala ya kijamii hali ambayo inawakosesha Amani katika kupata majukumu yao ya msingi hivyo ipo haja kwa jamii kushirikiana kwa pamoja katika kuwasaidia walemavu wa macho.

“Walemavu wa macho wanapitia changamoto nyingi   ikiwemo kukosa mashirikiano kwa baadhi ya wanajamii hususani katika masuala ya kijamii hali ambayo inawakosesha Amani katika kupata majukumu yao ya msingi hivyo ipo haja kwa jamii kushirikiana kwa pamoja katika kuwasaidia walemavu wa macho” amesema Bimaryam.

Naye Waziri afya Zanzibar Muheshimiwa Nassour Ahmed Mazrui amekipongeza kikundi hicho kwa kutoa elimu juu ya umuhimu wa kutunza macho kutokana na umuhimu wa kiungo hicho kwani kufanya hivyo kutapelekea  kuepuka ulemavu wa kudumu.

Hata hivyo Mh Mazrui ametoa wito kwa jamii kushirikiana kwa pamoja kuwasaidia walemavu wa macho ili kuepukana na changamoto zinazowakabili katika jamii zao.

Nao walemavu wa macho waliokuwepo katika uzinduzi huo wamesema kuwa wamefarijika kuwepo katika uzinduzi huo pamoja na kuishauri  jamii kutokutumia mitishamba pindi wanapoumwa na macho na badala yake kufika katika vituo vya afya ili kupata ushauri wa Daktari na matibabu Zaidi.

Vile vile wametoa wito kwa wanajamii wenye watoto ambao ni walemavu wa macho kutowafungia ndani na badala yake kuwatoa ili waweze kupata haki kama watoto wengine.

Washiriki kutoka walokuwepo katika uzinduzi huo wamefurahishwa na ubunifu wa uhamasishaji wa maradhi hayo kwani ni jambo la kupongezwa kwa kikundi hicho kwa ubunifu wao waliyoufanya wa kupeleka ujumbe kwa njia ya muziki ambao utapelekea jamii kuupata kwa haraka Zaidi.



No comments