Breaking News

TAMWA ZNZ YAWAWEZESHA WAANDISHI WA HABARI KUANDIKA HABARI ZA KUKABILIANA NA MABADILIKO YA TABIANCHI KWA MUKTADHA WA USAWA WA JINSIA NA UONGOZI

 Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania – Zanzibar (TAMWA ZNZ) kimeendesha mafunzo maalum kwa waandishi wa habari ili kuwaongezea uelewa wa kuripoti habari za mabadiliko ya tabianchi kwa kuzingatia mchango wa wanawake katika kulinda mazingira na kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Akifungua mafunzo hayo, Meneja Programu wa TAMWA ZNZ, Nairat Abdulla Ali, amesema mafunzo hayo yamelenga kujenga uwezo wa waandishi wa habari kuandika habari zenye mtazamo wa wa jinsia, hasa katika maeneo ya kilimo mseto, uhifadhi wa mikoko, usawa wa kijinsia na nafasi ya wanawake katika uongozi wa masuala ya mazingira na umiliki wa ardhi.

“Kuna maeneo ambayo yako ndani ya mradi wetu lakini waandishi wengi bado hawajafikia kuyaandika kwa kina kutokana na uelewa mdogo. Mafunzo haya yatawasaidia kuona maeneo haya kwa upana na kuyapa kipaumbele katika kazi zao za kila siku,” amesema Nairat Haji.



Ameongeza kuwa ni dhamira ya TAMWA ZNZ kuhakikisha waandishi wa habari wanakuwa na uelewa wa kina wa usawa wa kijinsia na uongozi, hasa kwa wanawake, katika jitihada za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ili jamii iweze kupata taarifa sahihi na zenye kuchochea mabadiliko chanya.

Akitoa mada kuhusu usawa wa kijinsia katika uandishi wa habari za mabadiliko ya tabianchi, kilimo mseto na uongozi, mkufunzi wa mafunzo hayo Ali sultani amewakumbusha waandishi wa habari kuzingatia maadili ya taaluma yao kwa kuhakikisha wanadumisha haki, usawa na kuheshimu utu wa watu wanaowaandika.

“Ni muhimu kuandika habari kwa lengo la kuibua changamoto na kuhamasisha ufumbuzi kwa jamii, si kwa nia ya kuwavunjia heshima au kuwadhalilisha,” amesisitiza Ali sultani.





Meneja wa Mahusiano ya Kimataifa kutoka Jumuiya ya Misitu Pemba (CFP) Lillian Simule, amesisitiza umuhimu wa waandishi wa habari kuzingatia usawa wa kijinsia wanaporipoti habari kuhusu mabadiliko ya tabianchi, kwani changamoto hizo haziwezi kutatuliwa kwa ufanisi bila kushirikisha ipasavyo wanawake na wanaume katika nafasi za maamuzi na utekelezaji wa mikakati ya mazingira.

Mafunzo hayo ya siku tatu ni sehemu ya juhudi za TAMWA ZNZ, Jumuiya ya misitu Pemba, (CFP) na Jumuiya ya misitu ya kimataifa (CFI) katika kuimarisha uwezo wa vyombo vya habari na wandishi wa habari Zanzibar kuripoti kwa weledi masuala yanayohusu mazingira, usawa wa kijinsia na maendeleo endelevu.

 



No comments