TAMWA-ZNZ Yawanoa Wanawake Wagombea Uongozi wa Kisiasa Zanzibar
Na Fatma Rajab
Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA-ZNZ) kimeendesha mafunzo ya siku tatu kwa wanawake wagombea uongozi kutoka vyama 14 vya siasa visiwani Zanzibar, kwa lengo la kuwawezesha kujenga ujasiri, kukabiliana na changamoto na kuendesha kampeni zenye ufanisi ili kuwavutia wapiga kura kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Akizungumza katika hafla ya kufunga mafunzo hayo, Mkurugenzi wa TAMWA-ZNZ, Dkt. Mzuri Issa Ali, amesema chama hicho kimegundua pengo lililopo kwa wanawake wanapogombea katika siasa ikiwemo kukatishwa tamaa, na kueleza kuwa muda umefika kuvivuka vizingiti vyote na kuchukua nafasi za uongozi majimboni. “Wanaume wengi wanapowaona wanawake wenye uthubutu na uwezo wa kuongoza, huonesha dharau kwa lengo la kuwavunja moyo na kuwarudisha nyuma. Ni muhimu wanawake kuungana, kushirikiana na kushikamana ili kuondoa mfumo dume na kufikia usawa wa kijinsia wa asilimia 50 kwa 50 katika uongozi wa kisiasa,” alisema Dkt. Mzuri.
Kwa upande wake, Dkt. Salum, akiwasilisha mada kuhusu mbinu za kushawishi wapiga kura, aliwataka wanawake wagombea kujiamini na kuandaa sera zenye mashiko na zinazotekelezeka. Alisisitiza kuwa wakati umefika kwa wanawake kuonesha uwezo wao katika kunadi sera kwa umakini ili kuvutia wapiga kura wengi.
“Utafiti wa kimataifa unaonesha kuwa wanawake wanapopewa nafasi za uongozi hufanya kazi kwa bidii, ni waadilifu na hujikita zaidi katika masuala ya kijamii na uimarishaji wa amani katika jamii,” alibainisha Dkt. Salum.
Naye Meneja Mawasiliano wa TAMWA-ZNZ, Bi. Saphia Ngalapi, akitoa mada kuhusu matumizi ya vyombo vya habari, aliwataka wagombea hao kutumia vyema majukwaa ya habari na mitandao ya kijamii kusambaza sera zao.
“Vyombo vya habari ni nyenzo muhimu inayowawezesha wagombea kufikisha ujumbe kwa umma kwa haraka na kwa wigo mpana. Pia mitandao ya kijamii ni jukwaa linalofuatiliwa na wapiga kura wengi, hivyo ni muhimu kuitumia kwa ubunifu katika kunadi sera zenye kuleta maendeleo,” alisema Bi. Saphia.
Akizungumza kwa niaba ya washiriki, Asiata Saidi Abubakari aliishukuru TAMWA-ZNZ kwa kuandaa mafunzo hayo na kueleza kuwa yamewaongezea uelewa na mbinu za kujilinda, kujiamini na kutumia vyombo vya habari kwa ufanisi.
“Maarifa tuliyoyapata yatatupa ujasiri na uthubutu wa kusimama imara katika kampeni, kuongeza idadi ya wapiga kura na kuchangia kufanikisha lengo la kufikia uwakilishi wa asilimia 50 kwa 50 katika nafasi za uongozi,” alisema Asiata.
Mafunzo haya ni muendelezo wa utekelezaji wa Mradi wa Kuwajengea Uwezo Wanawake Kisiasa (SWILL) unaotekelezwa na TAMWA-ZNZ, PEGAO, JUWAUZA, na ZZAFELA, kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo kutoka Norway, wenye lengo la kuongeza ushiriki wa wanawake katika siasa na uongozi wa kitaifa.

No comments