Breaking News

MWANAMKE SHUPAVU KUTOKA MAGHARIB "B" UNGUJA AIBUKA KUWA SAUTI YA WANAWAKE NA VIJANA

 


Na Thuwaiba Habiu


"Wanawake wa Zanzibar, sasa ni wakati wenu kuamka, kuungana, na kuingia katika siasa kwa nguvu zote. Hatuwezi tena kukaa pembeni tukitamani  uongozi baada ya kuendesha mustakabali wetu wenyewe.”

Ni sauti mwanamke jasiri anayesimama kidete leo katika siasa za Unguja, jimbo la Pangawe. akitoa wito usio wa kawaida kwa wanawake wenzake  wenye  kuashiria mapambano, ya kuondoa vizingiti vya ubaguzi, uonevu wa kijinsia, juu ukosefu wa fursa kwa wanawake na vijana.

Mwanamke huyu ametoka katika jamii ambayo mara nyingi nafasi za uongozi huzingatiwa kuwa ni za wanaume, na kuwanyima wanawake uhuru wa kuwa viongozi



Historia yake

Huyu ni Bi Ghanima  Omar Sultan

amezaliwa Kisiwani Pemba, katika eneo la Biti Abeid, Chake Chake. kwa sasa ni mkaazi wa Muembe  Majongoo  Unguja.

Elimu yake ya msingi aliipata katika Skuli ya Raha Leo, ambako alisoma kutoka darasa la kwanza hadi la saba na hakubatika kumaliza elimu ya sekondari kutokana na kuolewa wakati akiwa kidatu cha tatu.

Licha ya maisha ya kawaida ya utotoni, leo hii, akiwa na umri wa miaka 54, Ghanima ni mmoja wa wanawake wachache wanaogombea ubunge kwa tiketi ya chama cha CUF katika Jimbo la Pangawe, Unguja.

Katika maisha ya ndoa, ameolewa na wanaume watano, na katika ndoa tatu kati ya hizo, alijaliwa watoto tisa. Japo changamoto za kifamilia zilikuwepo, hazikumzuia kusimama kidete na mapambano ya kuwakomboa wanyonge hususan wanawake na vijana.



Safari ya kisiasa

Katika safari yake ya siasa Bi. Ghanima alianza kushiriki siasa rasmi mwaka 1993 akiwa miaka 30 kama mwanachama wa kawaida katika chama cha  CUF na alijiunga na kikundi cha hamasa.

Tangu wakati huo, amekuwa mstari wa mbele katika masuala ya siasa. Mwaka 1997 alichaguliwa kuwa Mjumbe wa Kamati Tendaji ya Wilaya ya Magharibi B  ambapo kwa wakati huo wilaya  hiyo ilianzia Mfenesini hadi Fumba na kuwa  Mjumbe wa Kamati ya Haki za Binadamu katika wilaya hio  hio. Mwaka 2005, alihudumu kama Mjumbe wa Jumuiya ya Wanawake ya Mkoa wa Magharibi B kwa muda wa miaka 10. Mwaka 2016, alichaguliwa tena kuwa Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa.

Baadaye alihamia ACT-Wazalendo na kugombea nafasi ya Mjumbe wa Kamati Tendaji ya Mkoa wa Magharibi B  nafasi aliyowahi kuitumikia hapo awali. Hata hivyo, baada ya uchaguzi wa ndani ya chama, alirudi tena CUF na kukaimu nafasi ya Katibu wa Wilaya ya Magharibi B. Hivi sasa, ni Katibu rasmi wa chama hicho na Mgombea wa Ubunge katika Jimbo la Pangawe.

Sababu ya kugombea

Nina uchungu na jimbo langu,” amesema kwa msisitizo. “Viongozi waliopita hawakuondoa vilio vya wananchi. Vijana wamejikuta katika makundi mabaya ya uvunjifu wa amani, kwa sababu hawana shughuli ya kufanya.”

Kwa sababu hizo, ameweka mbele ajenda ya kuwawezesha vijana kwa:

Kuwawekea mazingira ya kufanya kazi,kuwapatia usafiri (gari) kwa ajili ya miradi,kuwatafutia wanasaikolojia wa kuwasikiliza na kuwashauri.

Kwa upande wa wanawake, Ghanima anaamini kuwa uchumi wa mwanamke ni silaha yake.

Na atapigania wanawake wapewe mikopo na mafunzo ya ujasiriamali, ili waweze kusimama kiuchumi.

“Mwanamke akiwezeshwa, jamii nzima inainuliwa. Siasa si uwanja wa wanaume pekee.” alieleza

Changamoto

Licha ya mchango wake mkubwa, amekumbwa na changamoto nyingi:

Kutengwa na baadhi ya wanachama waliomwona msaliti baada ya kuhama chama cha Act  wazalendo  na kurejea CUF.

Sheria kandamizi za baraza la wakilishi zinakwaza wagombea wapya  kwa kuwekewa  marufuku ya kubandika mabango mitaani sasa hii inawakosesha wanawake kujitangaza.

Mfano wa kuigwa

Ghanima anasema alihamasishwa kuingia katika siasa na marehemu Bi Khadija Salum Ali ‘Makotena’, aliyekuwa Mbunge wa viti maalum kwa miaka 15 katika chama cha Mwananchi CUF

 Akiwa katibu wake, alijifunza thamani ya uongozi wa kibinadamu, huruma, na mshikamano.

Leo hii, Ghanima anaamini katika usawa wa kijinsia:

“Nataka kuona asilimia 50 kwa 50 kati ya wanaume na wanawake katika uongozi. Haki hii si zawadi ni haki yetu ya msingi.”



Wito kwa Wanawake

Kupitia historia yake, Bi Ghanima anawataka wanawake wasisubiri kusukumwa wajisukume wenyewe. Asilimia kubwa ya wanawake wana ndoto, lakini wanazizuia kwa hofu au vizingiti vya kijamii.

“Wanawake wajiamini. Wasiogope vikwazo. Dunia ya sasa inahitaji wanawake wanaojua thamani yao.”

“Ikiwa tunaweza kulea watoto, tunao uwezo wa kulea majimbo, mikoa na hata taifa.”

Pia nahimiza wanawake kusimama wenyewe na kutokubali kudhalilishwa.

“Hakuna mafanikio ya kweli ikiwa unategemea mgongo wa mtu mwingine,” anaeleza

Naamini kuwa siasa na mapenzi havichangamani, na ili mwanamke afanikiwe, lazima ajitambue na asimame kwa miguu yake.



No comments