Breaking News

TAMWA ZNZ NA WADAU WENGINE ZANZIBAR WAJADILI MUSTAKBALI SHERIA NA UHURU WA HABARI.

 


Na Fatma Rajab 

Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Zanzibar (TAMWA-ZNZ) kimefanya mkutano wa kutoa mrejesho wa utekelezaji wa programu ya mapitio ya sheria za habari na uhuru wa habari, kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali wa sekta ya habari visiwani Zanzibar.

Akifungua mkutano huo, Afisa Ufuatiliaji na Tathmini kutoka TAMWA-ZNZ, Mohammed Khatib, katika ofisi za chama hicho Mkanjuni kisiwani Pemba, amesema mkutano huo ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha uwazi, ushirikishwaji na kuimarisha sauti ya wandishi wa hahabari katika mchakato wa mabadiliko ya sheria za habari Zanzibar.

“Kwa kipindi chote cha utekelezaji wa programu hii, tumeweza kufikia hatua muhimu katika kuhamasisha majadiliano ya kina kati ya waandishi na wadau wa habari na watoa maamuzi. Ripoti tunayowasilisha leo inaonesha hali halisi ya sasa, mafanikio, lakini pia maeneo yanayohitaji maboresho,” amesema Mohammed Khatib, Afisa Ufuatiliaji na Tathmini (TAMWA ZNZ).

Akiwasilisha ripoti  hiyo, afisa program wa mapitio ya sheria za habari na uhuru wa habari kutoka TAMWA-ZNZ  Zaina Mzee, ameelezea  juhudi za ushawishi zilizofanywa na (TAMWA ZNZ), ambazo ni pamoja na mikutano na baadhi ya Wawakilishi wa Baraza la Wawakilishi Zanzibzr, mafunzo kwa wandishi wa habari kuhusu sheria za habari, na kampeni za uelimishaji kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.

Sambamba na hilo, programu hii imewawezesha waandishi 25 kutoka Unguja na Pemba kupata mafunzo ya kina juu ya namna ya kuchambua na kuripoti sheria za habari, hasa zile zenye vifungu vinavyominya uhuru wa vyombo vya habari.





Nao washiriki wa mkutano huo wametoa maoni na mapendekezo ya kuboresha ripoti, huku wengi wakisisitiza umuhimu wa kuwa na sheria mpya ya habari inayolinda uhuru wa vyombo vya habari, haki za waandishi wa habari, na uwajibikaji wa kitaaluma.

Pia wameleza jinsi mafunzo hayo yalivyowawezesha kubadili mitazamo yao kiuandishi.

“Kwa mara ya kwanza tumeelewa kwa undani jinsi sheria za habari zinavyoweza kuathiri uhuru wetu wa kuripoti. Mafunzo haya yametupa ujasiri wa kuuliza maswali mbalimbali kwa viongozi bila woga, kwa sababu sasa tumeelewa haki zetu kama wandishi wa habari,”

Aidha wamesisitiza umuhimu wa kuendelea kushirikiana kama wadau na kuendeleza uchechemuzi ili kuharakisha mchakato wa upatikanaji wa sheria mpya, kwa kuzingatia mazingira ya sasa ya kidijitali na changamoto zinazowakumba waandishi wa habari Zanzibar.

Mkutano huo umefanyika katika ofisi za TAMWA-ZNZ zilizopo Mkanjuni, Chake Chake -Pemba, na umewaleta pamoja waandishi wa habari, wanaharakati wa vyombo vya habari, wawakilishi wa asasi za kiraia, na wadau wa maendeleo kwa lengo la kujadili mafanikio na changamoto zilizojitokeza katika utekelezaji wa programu hiyo kwa kipindi cha mwaka 2024-2025


No comments