NI IPI HATMA YA KESI ZA UJAUZITO/ BINTI WAELEZEA MACHUNGU WANAYOPITIA.
“Hali yangu ni ya uhitaji mkubwa sina uwezo wa kifedha kumsaidia mjukuu wangu ajifungue salama, naiomba jeshi la polisi kunisaidia na kuhakikisha mtuhumiwa anakamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.”
Huyo ni Bi Miza Khalfan sio jina lake halisi ni mlezi wa mtoto wa miaka 14 ambaye alibakwa na kupewa ujauzito, alizungumza kwa uchungu mkubwa akieleza hali ngumu ya kiuchumi anayopitia, Akionekana mwenye majonzi, bibi huyo anaeleza kuwa tukio hilo limeumiza sana familia yao kwani limemkatisha masomo mjukuu wake ambaye alikuwa na ndoto kubwa za kimasomo. Anasemasema kuwa mara baada ya mtuhumiwa kupata taarifa kuwa binti huyo ni mjamzito, alitoroka na kwenda kusikojulikana, jambo linaloongeza ugumu wa kupatikana kwa haki.
Bi Miza sio jina lake halisi ni miongoni mwa wengi ambao wanakumbwa na Kesi za ukatili zinazohusisha kubakwa na kupewa ujauzito, ambapo mara nyingi hukumbwa na changamoto kubwa za kisheria na ushahidi. Moja ya changamoto kuu ni kuthibitisha bila shaka yoyote kuwa mtuhumiwa ndiye aliyebaka na kusababisha ujauzito. Jambo linalopelekea kesi hizo kuishia bila kupata haki.
Mlezi huyo aliomba msaada wa haraka kutoka kwa serikali na vyombo vya sheria ili kuhakikisha mjukuu wake anapata haki zake za msingi ikiwemo elimu, hasa ikizingatiwa kuwa familia haina uwezo wa kugharamia huduma za afya na mahitaji ya uzazi salama, kutokana bibi huyo kuishi peke yake ambapo wazazi wa binti aliyebakwa washafariki pia bibi huyo hana kazi ya uhakika kujipatia kipato cha kukidhi mahitaji ya familia yake.
Kwa mujibu wa takwimu za Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali (OCGS) Zanzibar, jumla ya matukio ya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia yaliyoripotiwa katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka 2022 hadi 2024 yalifikia 5,123. Kati ya kesi hizo, ni 845 pekee ndizo zilizoshinda mahakamani, sawa na asilimia 16.5 ya kesi zote zilizoripotiwa. Hali hii inaonyesha kuwa ingawa kuna ongezeko la kuripoti matukio ya ukatili wa kijinsia, bado kiwango cha upatikanaji wa haki kwa waathiriwa ni mdogo, jambo linaloashiria kuwepo kwa changamoto katika ushughulikiaji na usimamizi wa mashauri ya aina hii.
ahanga wa matukio hayo hufikia hatuwa ya kukata tamaa ya kushiriki mambo ya kijamiii kwa kujiona kama wamefedheheka na wengine kushindwa hata kupata haki zao za msingi ikiwemo Elimu kwakuhofia jamii itawacheka na kuwadharau ama kuwatenga wasiwe sawa na wenziwao.
Nairat Ali sio jina lake halisi ni mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 14 aliyebakwa na kugundulika akiwa na ujauzito wa miezi mitano alikatisha masomo baada ya wenziwe umcheka kumsimanga kwa hali iliyompata.
"Baada ya kugundulika nina ujauzito wanafunzi wenzangu walianza kunicheka na kunichokoza, niliacha skuli, lakini natamani kuendelea na masomo yangu ila sio palepale nataka nihamishiwe sehemu nyengine”.
Alisema binti huyo kwa huzuni macho yake yalibubujika machozi, alinyanyua mkono wake wa kulia na kukamata ncha ya Kanga aliyojitanda alipeleka machoni na kujifuta machozi na mkono mwengine wa kushoto aligusa tumbo lake taratibu aliyainamisha macho yake chini.
Huyo ni Mwanafunzi wa darasa la saba, Binti wa miaka 14 mkaazi wa Shehia ya Kidimni wilaya ya kati Unguja anaedaiwa kubakwa mwishoni mwa mwaka 2024 na kugundulika kuwa na ujauzito wa miezi mitano baada ya hali yake ya afya kudhoofika na kupelekwa hospital kwa vipimo.
Ni wazi kuwaonya watu hao ni sawa na kumpigia mbuzi gitaaa kwa maana vitendo hivyo vichafu vinashamiri kila leo na hao wanao shiriki vitendo hivyo hawajali bali kuendekeza matamanio yao ya kimwili bila kujali hisia, maumivu, mateso na majuto watakayopitia wanao watendea unyama huo.
Binti huyo anaedaiwa kubakwa na kupewa ujauzito alieleza kuwa “siku ya tukio nilipokwenda skuli nilifatwa na mtu aliyemsemesha maneno ya kumtaka lakini nilimkatalia”, alisisitiza kwa kusema “baada ya masomo ya ziada nilipokwenda chooni nilimkuta mtu huyu amejificha na ndipo aliponibaka”.
Ingawa yote hayo yalitokea bado mtoto huyo aliendelea kukaa kimya bila kumwambia yeyote hadi baada ya miezi mitano kugundulika kuwa ni mjamzito, ambapo kwa kesi za ubakaji tayari zimepoteza ushahidi wa awali na wenye mashiko kutia hatiani mtuhumiwa.
Mwalimu mkuu wa skuli ya Kidinmni Muhammed Aboud Juma alihimiza jamii “kuwa karibu na watoto wao na kuishi nao kirafiki ili kujuwa mienendo na mabadiliko yao mapema ili kuchukua hatua zinazostahiki kwa wakati. Aidha amewaasa wazazi na walezi kuacha tabia ya ukali na kuwatisha watoto jambo ambalo huwafanya wawe wasiri na kuficha vikwazo wanavyokutana navyo katika maisha yao ya kila siku.
Aidha alitumia nafasi hiyo kumtaka binti huyo kujitokeza kufanya mtihani wake wa mwisho wa darasa la saba kisha kuendelea na masomo baada ya kujifungua.
Alitilia mkazo Mwalimu mshauri wa skuli aliyosoma binti huyo Kaeni Issa Pandu kwamba “tulipopewa taarifa tuliwasilisha Wizara ya Elimu na sasa tuna mpango wa kumsaidia arudi skuli ili akamilishe mtihani wa darasa la saba”.
Ofisi ya ustawi wa jamii wilaya ya kati nayo ilisimama kidete kutetea haki ya Binti huyu ambapo Ali Shehe Kombo kutoka Ofisi hiyo alisema ofisi yake tayari imempleka muathirika hospitali na kituo cha polisi kwa ajili ya huduma na matibabu na hatua zaidi za kisheria, vile vile alitilia mkazo na kusema “tumeambiwa mtuhumiwa kakimbia sasa tunasubiri polisi kukamilisha ufuatiliaji”.
kwa upande wake mwanaharaki wa kupinga ukatili na udhalilishaji Matheo Herman alisisitiza “elimu endelevu kwa jamii na kutoa wito kwa wazazi, watoto na viongozi wa mitaaa kuripoti matukio kama hayo bila ya kuficha ili wahusika wachakuliwe hatua za haraka”.
Aidha amesisitiza kuwa kuna kila haja kwa jamii kuishi kwa ushirikiano katika kuwalinda watoto dhidi ya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia, kwani mapambano haya ni yanahitaji nguvu ya pamoja kwani kidole kimoja hakivunji chawa.
Afisa Programu chama cha Waandishi wa habari Tanzania zanzibar (TAMWA ZNZ) Asia Makame ameisisitizajamii kuwapa elimu rika ya namna ya kujikinga na ukatili na udhalilishaji watoto tokea wakiwa wadogo ili wawe wawazi kueleza mambo hayokwa kujiamini pindi yanapotokea.
“ulezi wa kirafiki na kumuelewesha mtoto namna ukatili na udhalilishaji wa kijinsia unavyotokea, njia za kujikinga, na kuripoti ndio vitajenga uthubutu kwa mtoto, tusipofanya hivyo watoto hujenga usiri na kuficha mambo yao” amesisitiza afisa huyo.
No comments