JAMII YATAHADHARISHWA KUWACHUKUWA WATOTO KWENYE MIKUTANO YA KAMPENI ZA KISIASA
Katika kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, wazazi na walezi wametakiwa kuacha tabia ya kuwachukua watoto kwenye mikutano ya kampeni za kisiasa. Taasisi za kijamii na za wanawake Zanzibar zimeonya kuwa kitendo hicho kinaweka watoto katika mazingira hatarishi kiafya na kiusalama, huku kikinyima haki yao ya malezi bora.
Taasisi hizo ni pamoja na JUWAUZA, PEGAO, ZAFELA, na TAMWA-ZNZ, ambazo kwa kushirikiana na Ubalozi wa Norway, zimeeleza kuwa mikutano ya kisiasa mara nyingi huhusisha msongamano, kelele na matendo yasiyofaa kwa watoto. Wameeleza kuwa watoto sio wapiga kura na uwepo wao kwenye mikutano hiyo hauna faida, bali huongeza hatari ya kufanyiwa vitendo vya udhalilishaji na ukatili.
Aidha taasisi hizo zimeeleza kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Mtoto Zanzibar Na. 6 ya 2011, kifungu cha 14(1) kinatamka wazi kuwa mtoto anatakiwa kulindwa dhidi ya mazingira yanayoweza kuhatarisha maisha au afya yake. Vilevile, Tanzania imeridhia mikataba ya kimataifa na kikanda ikiwemo Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Watoto (CRC) na Mkataba wa Afrika wa Haki na Ustawi wa Mtoto (ACRWC) ambayo inasisitiza ulinzi na ustawi wa watoto.
Takwimu kutoka Afisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali (OCGS) zinaonyesha kuongezeka kwa matukio ya ukatili na udhalilishaji dhidi ya watoto kila mwezi ambapo kwa mwezi wa Juni 2025 kulikuwa na matukio 97, ambapo matukio 83 sawa na asilimia (85.6%) walikuwa watoto, pia kwa mwezi wa Julai 2025 Matukio ya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia yalikuwa 107, ambapo waathirika watoto walikuwa 95 sawa na asilimia (88.8%) na kwa mwezi Agosti 2025 Matukio hayo yalikuwa 116,na waathirika watoto ni 104 (89.7%).
kutokana na kuongezeka kwa matukio hayo JUWAUZA, PEGAO, ZAFELA na TAMWA-ZNZ wamewataka viongozi wa kisiasa, viongozi wa dini, wazazi, walezi na vyombo vya habari kushirikiana katika kutoa elimu na kuchukua hatua za kuwalinda watoto dhidi ya vitendo vya udhalilishaji na ukatili.
No comments