VIJANA WATAKIWA KUTUMIA FURSA ZILIZOPO KUJIKWAMUA KIUCHUMI.
NA NISHAN KHAMIS
Vijana wa Mkoa wa Kaskazini Unguja wametakiwa kuzikimbilia na kuzitumia ipasavyo fursa zilizopo katika mkoa huo, ikiwemo sekta ya bahari, utalii, uvuvi, kilimo, biashara na ujasiriamali, ili kujikwamua kiuchumi na kuongeza mchango wao katika maendeleo ya jamii.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Jumuiya ya Vijana na Elimu Wilaya ya Kaskazini A (JUVIEKA), Mbarouk Maalum Mohammed, wakati akizungumza katika mafunzo ya siku tatu yaliyowakutanisha vijana 30 kutoka Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Mafunzo hayo yameandaliwa na JUVIEKA kwa ufadhili wa Shirika la ActionAid Tanzania na kufanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kituo cha Walimu Mkwajuni, Wilaya ya Kaskazini A, yakilenga kuwajengea vijana uwezo katika ushawishi na utetezi wa sera pamoja na ushiriki katika harakati za kijamii.
Mbarouk amesema Mkoa wa Kaskazini Unguja una fursa nyingi zinazoweza kuwa chanzo cha ajira na kipato kwa vijana, hivyo ni muhimu kwao kuwa na uelewa, ubunifu na maarifa ya kuzitambua na kuzitumia fursa hizo.
Amesema sekta ya bahari na utalii ni miongoni mwa maeneo yenye nafasi kubwa kwa vijana, sambamba na uvuvi, kilimo, biashara, huduma na shughuli mbalimbali za ujasiriamali zinazoweza kuwawezesha vijana kujenga maisha yao kiuchumi.
Aidha, amesema vijana wanapaswa kushiriki kikamilifu katika mijadala ya kijamii na kisera ili waweze kuelewa sera zinazowahusu, kuibua changamoto zinazowakabili na kushawishi mabadiliko yenye manufaa kwa jamii.
Mbarouk amesema mafunzo hayo yamewajengea vijana uwezo wa kutambua mbinu za ushawishi na utetezi, kuelewa nafasi yao katika michakato ya sera na kuongeza ushiriki wao katika ngazi mbalimbali za maamuzi.
Ametoa wito kwa vijana kutumia maarifa waliyoyapata kwa vitendo, kuwa sauti ya wenzao, kufuatilia fursa zilizopo katika maeneo yao na kutumia ujuzi walionao katika kujenga ajira na shughuli za kiuchumi.
Kwa upande wao, vijana walioshiriki mafunzo hayo wamepongeza JUVIEKA na ActionAid Tanzania kwa kuwawezesha kupata maarifa na ujuzi, wakisema mafunzo hayo yamewasaidia kutambua nafasi na wajibu wao katika masuala ya sera, jamii na maendeleo.
Mafunzo hayo ni sehemu ya jitihada za JUVIEKA kwa ufadhili wa ActionAid Tanzania za kuwawezesha vijana kushiriki kikamilifu katika michakato ya kijamii na kisera, huku wakitumia fursa zilizopo katika maeneo yao kwa ajili ya kujenga maisha bora na kuchangia maendeleo ya jamii.



No comments