Breaking News

WADAU WA MAENDELEO YA VIJANA WATAKIWA KUSHIRIKIANA MAADHIMISHO YA SIKU YA VIJANA .

 


NA SITI ALI.

Wadau wa Maendeleo ya Vijana Zanzibar wametakiwa kushirikiana kwa pamoja ili kuhakikisha Maadhimisho ya Siku ya Vijana Kimataifa 2026 yanafanyika kwa mafanikio na kuleta matokeo chanya kwa maendeleo ya vijana nchini.

Wito huo umetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Vijana, Ajira na Uwezeshaji, Nd. Salama Mbarouk Khatib, wakati akifungua kikao cha uratibu wa Maadhimisho ya Siku ya Vijana Kimataifa kilichofanyika katika Ukumbi wa Wizara, Mpendae.

Katibu Mkuu amesema ushirikiano wa wadau ni msingi muhimu wa kufanikisha maadhimisho hayo, akieleza kuwa kila taasisi ina nafasi ya kutoa mchango wake katika kuwajengea vijana uwezo na kuhamasisha ushiriki wao katika maendeleo ya taifa.

Amewahimiza vijana kushiriki kwa wingi katika shughuli zote zilizopangwa kuanzia tarehe 6 Agosti na kufika kwa wingi katika kilele cha maadhimisho kitakachofanyika tarehe 12 Agosti katika Ukumbi wa Golden Tulip Hotel.

Aidha, amewapongeza wadau wa maendeleo ya vijana kwa juhudi wanazozifanya katika kuwawezesha vijana kupitia programu mbalimbali zinazochangia maendeleo yao ya kiuchumi, kijamii na kitaaluma.



Katibu Mkuu ametumia fursa hiyo kuwakumbusha vijana umuhimu wa uzalendo, akisema kuwa maendeleo ya taifa yanategemea vijana wenye maadili mema, uwajibikaji na mapenzi ya kweli kwa nchi yao.

"Nchi inahitaji vijana wazalendo. Kijana mzuri ni yule anayependa nchi yake, hapendi kuharibu maisha yake na ya wengine," amesema Nd. Salama Mbarouk Khatib huku akisisitiza umuhimu wa kulinda amani na mshikamano wa taifa.

Vilevile, amezitaka kamati zote zilizoundwa kwa ajili ya kuratibu maadhimisho hayo kutekeleza majukumu yao kwa weledi, kushirikiana kwa karibu na kuwasilisha taarifa za utekelezaji mara baada ya kumalizika kwa maadhimisho.

Akimkaribisha Katibu Mkuu, Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Vijana Zanzibar, Nd. Shaib Ibrahim Muhamed amesema maandalizi ya maadhimisho hayo yanaendelea vizuri na kwamba Wizara imejipanga kuhakikisha vijana wanashiriki kikamilifu katika shughuli zote.

Shaib ameishukuru Wizara ya Vijana, Ajira na Uwezeshaji kwa usimamizi na maelekezo yake, huku akibainisha kuwa maadhimisho ya mwaka huu yatahusisha shughuli mbalimbali zikiwemo vijana na afya, vijana na ubunifu, vijana na mazingira, vijana na ushiriki, ushirikishwaji pamoja na uzalendo.

Kwa upande wake, Afisa Uratibu na Ufuatiliaji wa Maendeleo ya Vijana, Nd. Maryam Omar Rashid, akiwasilisha ratiba ya shughuli za taasisi mbalimbali, amezitaka taasisi zote kutekeleza majukumu yao kwa wakati, kwa uwajibikaji na kwa mashirikiano ili kufanikisha malengo ya maadhimisho hayo.

Nao wadau wa maendeleo ya vijana wameipongeza Wizara kwa kuwashirikisha katika kila hatua ya maandalizi, wakiahidi kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa shughuli zote zilizopangwa.


 Maadhimisho ya Siku ya Vijana Kimataifa 2026 yanabebwa na kaulimbiu isemayo, "Mazingira tofauti, dhamira moja kwa taifa."


1 comment: