Breaking News

ZANZIBAR KUIMARISHA VIWANJA VYA NDEGE NA BANDARI KUKIDHI VIGEZO VYA KIMATAIFA

 


NA SITI ALI

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuimarisha miundombinu ya Viwanja vya ndege nchini ili viendelee kukidhi viwango vya Kimataifa

Hayo yameelezwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akiwa katika muendelezo wa ziara yake ya kukagua miradi mbali mbali ya maendeleo inayojengwa Zanzibar.

Amesema kukamilika kwa ujenzi wa kituo cha biashara na jengo la abiria la Terminal two, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa  Abeid Amani Karume (AAKIA) utakuwa ni miongoni mwa viwanja bora duniani kwa utoaji wa huduma bora kwa wageni wanaoingia na kutoka Zanzibar.

Amesema uwanja wa ndege ni lango kuu la ukuwaji wa uchumi wa nchi ambao hutokana na kuongezeka kwa ajira, kuongezeka kwa Idadi ya watalii wanaoingia Zanzibar sambamba na  kuongezeka kwa mapato ya Taifa.



Mhe. Hemed amewapongeza wafanyakazi wa Mamlaka ya Uwanja wa ndege kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa wageni wanaoingia nchini jambo linalozidi kuipa heshima Zanzibar Kimataifa.

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhe. Dkt Khalid Salum Muhammed amesema utakapokamilika ujenzi wa majengo hayo uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Zanzibar utakuwa na uwezo wa kuhudumia abiria Milioni 3 kwa mwaka ambapo utakuwa na uwezo wa kukidhi ongezeko la watalii wanaoingia nchini.

Dkt. Khalid amefahamisha kuwa Majengo hayo yanatarajiwa kukamilika kabla ya mashindano ya Afkon yanayotarajiwa kufanyika mwakani na kutoa fursa kwa wageni kuweza kupata huduma mbali mbali wafikapo nchini.

Kwa upande wake Mhandisi  EMANUEL HOLEHOLE EXAVERY amesema majengo hayo yapo katika hatua za mwisho kukamilika ambapo yamejumuisha jengo la ghorofa tatu kwa ajilili ya ofisi za wafanyakazi, jengo la abiria, majengo ya huduma za kibenki, majengo mawili kwa ajili ya migahawa na sehemu ya maegesho ya magari kwa ajilinya wafanyakazi, wageni na wananchi wanaongia uwanjani hapo kufuata huduma mbali mbali.

Mhandisi HOLEHOLE amesema uwekezaji huo utakwenda kutoa matokeo chanya kwa kuongezeka kwa sehemu za kufanyia biashara uwanjani hapo, mazingira bora kwa wafanyakazi pamoja na kuimarika kwa utowaji wa huduma kwa wageni na wazawa watakaodafiri kupitia Uwanja wa Ndege wa Zanzibar. 

Akikagua kituo cha ushushaji na upimaji wa mafuta pamoja na bandari jumuishi ya Mangapwani, Mhe. Hemed amesema upatikanaji wa Nishati ya Mafuta unazidi kuimarika kutokana na usimamizi madhubuti wa mamlaka husika pamoja na kutoa huduma kisasa jambo linalopunguza mianya ya upotevu wa nishati hio.

Adha, Mhe. Hemed amelitaka Shirika la Bandari Zanzibar pamoja na kampuni wanazoshirikiana nazo katika kufanya kazi kuhakikisha kazi  ambazo zinaweza kufanywa na wazawa wapewe nafasi hizo endapo watakidhi vigezo ili kuwapa ari ya kuendelea kuwa wazalendo kwa Taifa lao.

Mapema Makamo wa Pili wa Rais alikagua ujenzi wa barabara ya Magereza hadi kinazini na kusema utakapokamilika ujenzi wa barabara hio yenye urefu wa kilomita 2.2 haitapendeza kuona watu wanaendelea kujenga na kufanya biashara katika maeneo ya hifadhi ya barabara jambo linalopelekea uharibifu wa miundombinu hio.



Amewataka wakandarasi na washauri elekezi wa ujenzi wa barabara zote zinazojengwa nchini kuhakikisha wanakamilisha kazi kwa wakati na kwa viwango vya hali ya juu ili miundombinu hio iweze kutumika kwa muda mrefu.

Katika ziara yake hio Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alikagua UJENZI WA JENGO LA BIASHARA NA JENGO LA ABIRIA LA TERMINAL TWO KATIKA UWANJA WA NDEGE WA ZANZIBAR, BARABARA YA MAGEREZA HADI KINAZINI, KITUO CHA KUSHUSHIA NA KUPIMIA MAFUTA MANGAPWANI, UJENZI WA BANDARI JUMUISHI YA MANGAPWANI PAMOJA NA BARABARA YA MFENESINI HADI MANGAPWANI


No comments