TALAKA NI CHANZO CHA MIGOGORO KATIKA FAMILIA SHEHIA YA KITOPE
NASITIALI.
Shehia ya Kitope, kama zilivyo jamii nyingi visiwani Zanzibar, inasifika kwa misingi yake ya tabia za kitamaduni, kidini na ujirani mwema. Hata hivyo, chini ya pazia hili la utulivu, kuna wimbi linalokua kwa kasi la kuvunjika kwa ndoa na kupelekea talaka.
Badala ya talaka kuwa suluhu ya amani pale wanandoa wanaposhindwa kuelewana, katika Shehia ya Kitope imekuwa chanzo kikuu cha migogoro mipya na mikubwa inayotikisa ustawi wa familia na jamii kwa ujumla. Hali hii inaifanya shehia kupoteza mshikamano wake wa asili na kuingiza chuki hadi kwa vizazi vinavyofuata.
Mkaazi wa Shehia ya Kitope, Bibi Laylat Kombo Omar, amesema wamekuwa wakikabiliwa na changamoto mbalimbali, hususan za utelekezaji wa watoto mara tu baada ya ndoa mpya kufungwa, jambo ambalo lina athari kubwa katika jamii.
"Katika mazingira ya Kitope, si jambo la kigeni kwa mwanaume kuoa mke mwingine baada ya kutoa talaka. Hata hivyo, ikiwa kuna watoto wa mke wa kwanza, kuingia kwa mke mpya mara nyingi huzua migogoro mipya ya urithi na upendeleo. Watoto wa mke aliyeachwa hujihisi kutengwa, jambo linalochochea uhasama wa kudumu dhidi ya baba yao na familia ya mke mpya," amesema Bibi Laylat.
Moja ya athari za haraka za talaka huko Kitope ni kuibuka kwa migogoro ya kiuchumi na mgawanyo wa mali. Mara nyingi ndoa zinapovunjika bila kuwepo mikataba rasmi ya kisheria au uelewa wa kutosha wa sheria za familia, suala la kugawana mali kama ardhi, nyumba au mashamba hugeuka kuwa chanzo kikuu cha migogoro.
Sheha wa Shehia hiyo, Bwana Ramadhani Said Abdallah, amesema wanawake wengi hujikuta wakiachwa bila makazi wala mtaji wa kujiendeleza, hali inayowalazimu kufungua malalamiko kwa viongozi wa shehia au mahakamani.
"Wanaume wengi baada ya talaka huacha kutoa matunzo ya watoto kama chakula, elimu na matibabu. Hali hii huzidisha chuki kati ya familia mbili zilizokuwa zimeunganishwa kwa ndoa," amesema Sheha huyo.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Wasaidizi wa Sheria Wilaya ya Kaskazini B, Shaaban Sariboko Makarani, amesema taasisi yao imekuwa ikipokea malalamiko mengi yanayohusu migogoro ya talaka na kutoa msaada wa kisheria, hasa kwa wanawake na watoto ambao ndio waathirika wakubwa.
"Watoto ndio waathirika wakuu wa migogoro endelevu baada ya talaka. Ndoa ikivunjika, malezi ya pamoja hutoweka na watoto hujikuta katikati ya mvutano wa wazazi. Mara nyingi hutumiwa kama silaha ya kulipizana kisasi. Mama anaweza kumzuia baba asiwaone watoto, huku baba naye akizuia msaada wa kifedha, jambo linalowaathiri watoto na jamii kwa ujumla," amesema Makarani.
Kwa upande wake, Imam katika Shehia ya Mahonda, Shehe Salum Gharib Salum, amesema migogoro ya talaka huchangia watoto kukosa maadili mema ambayo ndiyo msingi wa maisha bora katika jamii.
"Ukosefu wa malezi kutoka kwa wazazi wote wawili huwafanya watoto wengi kujiingiza katika makundi yasiyofaa, kutoroka shule na wakati mwingine kujihusisha na vitendo vinavyowagonganisha na sheria. Hali hii hurudisha nyuma maendeleo ya familia na jamii," amesema Shehe Salum.
Tatizo la migogoro ya talaka ni miongoni mwa mambo yanayochangia kuongezeka kwa baadhi ya kesi za udhalilishaji zinazorudisha nyuma ustawi wa jamii na kuzalisha kizazi kisicho na maadili pamoja na kukosa malezi bora.
Kwa mujibu wa takwimu za Mahakama ya Mkoa wa Kaskazini Unguja, zilizotolewa na Hakimu Luciano Makwenyengo, mwaka 2025 jumla ya kesi 31 za udhalilishaji ziliripotiwa. Kati ya hizo, kesi 25 zilimalizika kwa kuachiliwa huru, kesi sita ziliendelea, watu saba walifungwa, watatu walitozwa faini, watu 14 walikuwa huru na kesi moja iliondolewa kutokana na mashahidi kutofika mahakamani kwa muda mrefu.
Aidha, kuanzia Januari hadi Mei mwaka 2026, jumla ya kesi 14 za udhalilishaji ziliripotiwa. Kati ya hizo, kesi nne zilimalizika, kesi 10 zinaendelea, mtuhumiwa mmoja alitozwa faini, mmoja alifariki dunia na kesi mbili ziliondolewa kutokana na mashahidi kutofika mahakamani kwa muda mrefu.
Kwa mujibu wa Mchungaji katika Shehia ya Kitope, Emmanuel Malingila, ndoa si jambo la watu wawili pekee bali ni muunganiko wa koo mbili, hivyo talaka huacha majeraha makubwa katika jamii nzima.
"Talaka inapogonga hapa Kitope, inabomoa daraja la undugu. Koo za pande zote mbili huanza kunyosheana vidole, kusitisha ushirikiano katika misiba, harusi na hata shughuli za kibiashara," amesema Mchungaji huyo.
Ili kunusuru Shehia ya Kitope dhidi ya janga hili la migogoro inayotokana na talaka, hatua mbalimbali zimeanza kuchukuliwa na wadau wanaosaidia jamii, wakiwemo Idara ya Maendeleo ya Kanisa Katoliki Jimbo la Zanzibar kupitia mradi wa Uwezeshaji wa Haki za Binadamu na Utawala Bora unaofadhiliwa na Misereor.
Afisa wa Ufuatiliaji na Tathmini wa mradi huo, Msafiri Thomas Mombo, amesema taasisi hiyo inaendelea kutoa elimu ya sheria kwa kushirikiana na Wasaidizi wa Sheria Wilaya ya Kaskazini B.
"Tunaendelea kutoa elimu kuhusu haki za wanawake na watoto baada ya talaka, hususan masuala ya matunzo na makazi ili kuzuia dhuluma zinazoweza kuzalisha kisasi. Pia tunaimarisha mabaraza ya usuluhishi kwa kushirikiana na Ofisi za Masheha pamoja na viongozi wa dini ili migogoro ipatiwe suluhu kabla ya kufikia hatua ya talaka.
Sambamba na hilo, tunaendelea kutoa huduma za ushauri wa kisaikolojia (counseling) kwa watoto na wazazi wanaopitia kipindi kigumu cha talaka ili kupunguza msongo wa mawazo unaoweza kusababisha hasira, fujo na ukiukwaji wa haki za binadamu," amesema Afisa Msafiri.
Kwa ujumla, talaka katika Shehia ya Kitope si mwisho wa ndoa pekee, bali ni mwanzo wa mlolongo mrefu wa migogoro unaovuruga amani ya familia na jamii. Ni wajibu wa kila mdau, kuanzia ngazi ya familia, viongozi wa dini, viongozi wa kimila na Serikali, kusimama kidete kulinda taasisi ya ndoa na kuhakikisha kuwa pale talaka inapokuwa suluhu pekee, inafanyika kwa heshima, haki na uwajibikaji bila kuacha majeraha ya kudumu kwa familia na jamii.


No comments