MRADI WA DIGITAL MALL ZANZIBAR SULUHISHO UKOSEFU WA SOKO KWA VIJANA.
NA SITI ALI.
Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Vijana Zanzibar, Shaib Ibrahim Mohammed, amesema kuwa mradi wa Digital Mall Zanzibar unatarajiwa kuwa suluhisho la changamoto ya ukosefu wa soko kwa vijana wanaojishughulisha na shughuli za uchumi wa buluu, hususan biashara za bidhaa zinazotokana na bahari.
Ameyasema hayo katika Ukumbi wa Nyumba ya Sanaa, Mwanakwerekwe, Zanzibar, wakati wa uzinduzi na utambulisho wa mradi huo kwa wadau mbalimbali wa Baraza la Vijana Zanzibar.
Amesema mradi huo utawapa vijana fursa ya kuuza bidhaa zao kupitia mfumo wa kidijitali, jambo litakalowawezesha kuwafikia wanunuzi wengi zaidi ndani na nje ya Zanzibar.
Kwa mujibu wake, matumizi ya teknolojia katika biashara yatasaidia kuongeza thamani ya mazao ya baharini, kuboresha ushindani wa bidhaa hizo na kuongeza kipato cha vijana wanaojihusisha na sekta ya uchumi wa buluu.
Ameeleza kuwa kupitia jukwaa hilo la kidijitali, vijana wataweza kutangaza bidhaa zao kwa urahisi, kupata taarifa za masoko kwa wakati na kujenga uhusiano wa moja kwa moja na wanunuzi bila vikwazo vya masoko ya kawaida.
Mkurugenzi huyo amewahimiza vijana wa Zanzibar kutumia kikamilifu fursa zitakazotolewa na mradi huo, akieleza kuwa ubunifu, matumizi ya teknolojia na ushirikiano ni nguzo muhimu za kujenga uchumi imara na kuongeza ajira kwa vijana.
Akimkaribisha mgeni rasmi, Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Zanzibar amesema mradi huo unalenga kuimarisha ushiriki wa vijana katika uchumi wa kidijitali sambamba na kukuza sekta ya uchumi wa buluu, ambayo ni miongoni mwa sekta zinazochangia maendeleo ya kiuchumi ya Zanzibar.
Ameongeza kuwa utekelezaji wa mradi huo utachangia kupunguza changamoto ya madalali, kuongeza uwazi katika biashara na kuwapa wajasiriamali vijana wanaojishughulisha na bidhaa za baharini fursa ya kupata masoko ya uhakika.
Naye Katibu Mtendaji wa Baraza la Vijana Zanzibar, Ali Haji Hassan, amesema kuwa mradi wa Digital Mall Zanzibar unatekelezwa na Baraza la Vijana Zanzibar (BVZ) kwa lengo la kuwajengea vijana uwezo wa kutumia teknolojia katika kukuza biashara zao na kuongeza ushindani wa bidhaa zao sokoni.
Amesema mradi huo utatoa mafunzo ya matumizi ya mifumo ya kidijitali, ujasiriamali na masoko, ili kuwawezesha vijana kutumia ipasavyo fursa zinazotokana na uchumi wa kidijitali.
Mradi huo unasimamiwa na Save the Children Tanzania na Taasisi ya Tanzania Bora Initiative kupitia ufadhili wa Umoja wa Ulaya ambao ni sehemu ya mradi wa Vijana Plus na kutekelezwa na Baraza la Vijana Zanzibar kwa kipindi cha miezi kumi na mbili.
Kupitia mradi huo, jumla ya vijana 1,600 watanufaika, ambapo asilimia 60 ni vijana wa kike na asilimia 3 ni vijana wenye ulemavu wanaojishughulisha na shughuli za baharini, hatua inayolenga kuhakikisha ushiriki jumuishi wa vijana katika maendeleo ya uchumi wa buluu na matumizi ya teknolojia nchini.
Wadau wa Baraza la Vijana walioshiriki kwenye shughuli hiyo wameupongeza uongozi wa Baraza la Vijana Zanzibar kwa juhudi wanazozichukua kuhakikisha Vijana wanainuka kiuchumi kupitia miradi inayoibuliwa na Baraza hilo

.jpeg)

.jpeg)
Ni nzuribikifanikisha hayo yote.
ReplyDelete