Breaking News

CEJG YATOA ELIMU YA SHERIA NA UTAWALA BORA KWA WILAYA YA KASKAZINI B ILI WANANCHI WAJUE HAKI NA WAJIBU WAO.

 



NA SITI ALI.

Kwa miaka mingi,jamii nyingi zimekuwa zikikabiliwa na changamoto ya uwelewa mdogo wa sharia,haki za binaadamu na utawala bora.Hali hiyo imechangia kuendelea kwa migogoro,vitendo vya ukatil,unyanyasaji na ubaguzi,huku wananchi wengi wakikosa uelewa wa namna ya kulinda haki zao na kupata msaada wa kishehia.

Kutokana na changamoto hizo,Idara ya Maendeleo ya Kanisa Katoliki Kanda ya Zanzibar kupitia Mradi wa Uwezeshaji wa Jamii kwa ajili ya Haki za Binaadamu na Utawala Bora Awamu ya Tano (CEJG Phase V)unaofadhiliwa na Misereor,imeendelea kutoa elimu ya msaada wa kisheria,haki za binaadamu na utawala bora katika shehiya ya Mahonda,Mkataleni Kitope,Donge Majenzi na Bumbwini Misufini,Wilaya ya Kaskazini B Unguja.



Mbali na kutoa elimu kwa wananchi,mradi huo unashirikiana na Wasaidizi wa Sheria Kaskazini B pamoja na kamati ya uwajibikaji na utawala bora ili kuimarisha ushiriki wa jamii katika kulinda haki za wananchi,kuhamasisha uwajibikaji na kurahisisha upatikanaji wa haki kwa wanawake,vijana,watoto na watu wenye ulemavu.

Kupitia mafunzo hayo,wananchi wameendelea kujifunza kuhusu haki zao za msingi,wajibu wao kama raia,umuhimu wa kushiriki kaika maamuzi ya maendeleo,pamoja na namna ya kuripoti vitendo vya ukatili,unyanyasajina ukiukwaji wa haki kwa kutumia mifumo iliyopo.

Afisa ufuatiliaji na Tathmini wa mradi huo Msafiri Thomas Mombo amesema uamuzi wa kuanzisha mradi ulitokana na matokeo ya tathmini iliyoonesha kuwa bado kuna uelewa mdogo wa sheria na haki za binaadamu katika baadhi ya jamii za Zanzibar.

Amesema wananchi wengi hawafahamu kikamilifu haki zao wala namna ya kuzitetea,jambo linalochangia kuendelea kwa migogoro na ukiukwaji wa haki za binaadamu kwa mujibu wake,kuwajengea wananchi uwezo wa kupata elimu ni hatua muhimu katika kujenga jamii inayozingatia usawa, Amani na utawala bora.

 “Wanawake wakipewa elimu sahihi katika shehiya wanakuwa rahisi kuelewa masuala ya haki,wajibu usawa na Amani katika maisha yao ya kila siku.”amesema Mombo.

Ameongeza kuwa utekelezwaji wa mradi utaendelea kutanuliwa ili wananchi wengi Zaidi waweze kunufaika,huku kamati pamoja na wasaidizi wa sheria wataendelea kuwa ni daraja muhimu la kuelimisha jamii kupitia mikutano, mijadala,na shughuli mbalimbali za kijamii.



Kwa upande wake Mwanasheria wa Mradi huo Peter Marwa,amesema kuanzishwa kwa mradi huo ni uwekezaji muhimu katika kujenga jamii inayo tambua haki na wajibu wake na kuimarisha upatikanaji wa haki pamoja na misingi ya utawala bora.

Ameeleza kuwa wananchi wataendelea kupewa elimu ya misingi ikiwemo haki ya elimu,haki ya kuishi bila ya ukatili, haki ya kushiriki katika maamuzi yanayowahusu aidha ameongeza kuwa elimu hiyo itawasaidia wananchi kuwa mabalozi wa haki katika familia na jamii zao.

Aidha amesema kuwa Zanzibar bado inakabiliwa na changamoto ya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia na ukiukwaji wa haki mbalimbali kutokana na hiyo kuna umuhimu wa kuwajengea uwezo wananchi wa kujilinda,kutoa taarifa wanapoona vitendo vya ukatili na kutafuta msaada wa kisheria kupitia taasisi husika.

Viongozi wa shehiya wameeleza kuwamafunzo hayo yameongeza uelewa wa wananchi kuhusu sharia na kupunguza mogogoro inayotokana na kutofahamu haki na wajibu wao.Sheha wa shehiya ya Mahonda Ali Issa Kinole,amesema elimu hiyo itawasaidia wananchi kuishi kwa kuzingatia sheria,maadili na kuheshimiana.

Naye Mkurugenzi wa Taasisi ya Wasaidizi wa Sheria Wilaya ya Kaskazini B Shaaban Sariboko Makarani,amesema kuwa Utawala Bora unahitaji Sheria kutekelezwa kwa usawa bila ubaguzi,huku makundi yote ya jamii yakipewa fursa sawa za kushiriki katika maendeleo.

“Utawala bora lazima za haki zitekelezwe bila ubaguzi wowote. Hakuna mtu au taasisi iliyo juu ya sheria, kuanzia viongozi wakuu hadi mwananchi wa kawaida. Hii inajumuisha pia ulinzi kamili wa haki za binadamu”ameeleza Sariboko.

Kwa upande wa Shehe na Imamu katika Shehiya ya Mahonda Shehe Salum Gharib Salum amesema kuwa elimu hiyo itawasaidia wananchi kuwaelimisha wenzao ili kujenga jamii inayoheshimu hakiza binaadamuna kupinga vitendo vya ukatili na unyanyasaji.

“Wanajamii waliopatiwa elimu hiyo watajitahidi kuwafundisha wenzao ili elimu hiyo izidi kuenea Zaidi katika shehia pamoja na jamii zinazowazunguka kwa manufaa ya nchi na taifa kwa ujumla.”ameeleza Shehe

Mnufaika wa mafunzo hayo kutoka Donge Majenzi Rehema Haji Seif amesema mafunzo hayo yamewawezesha kuelewa haki zao na kuwapa ujasiri wa kutumia mifumo ya kisheria kutafuta haki wanapokumbana na changamoto.

“Tunashukuru kanisa katoliki kanda ya Zanzibar kupitia Mradi wa Uwezeshaji wa Haki za Binadamu na Utawala Bora kwa kutupatia mafunzo haya kwani tumepata uwelewa wa kutosha juu ya masuala ya haki na sheria na kuziomba shehia kuwa sehemu salama kwa wananchi kupeleka malalamiko yetu bila ya hofu na vitisho”ameeleza Rehema.

Kwa ujumla utekekelezwaji wa mradi huo wa uwezeshaji wa jamii kwa ajili ya Haki za Binaadamu na Utawala Bora Awamu ya Tano unaonesha dhamira ya Idara ya Maendeleo ya Kanisa Katoliki Kanda ya Zanzibar ya kujenga jamii inayotambua haki na wajibu wake,inayoshiriki kikamilifu katika utawala bora na inayoheshimu misingi ya haki za binaadamu.Kupitia elimu ya msaada wa kisheria,uhamasishaji jamii na ushirikiano na viongozi wa serikali,viongozi wa dini na wadau mbali mbali wa maendeleo,mradi unaendelea kuweka msingi wa jamii yenye Amani,usawa,uwajibikaji na maendeleo endelevu Zanzibar.

Mwisho.

 

 

 

 

 

 

 


No comments