MFUMO WA LARIS KUSAIDIA KUTATUA CHANGAMOTO ZA ARDHI ZANZIBAR.
NA SITI ALI
Kuanzishwa kwa Mradi wa Mfumo wa usimamizi na usajili wa taarifa za ardhi (LARIS) utasaidia kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi katika sekta ya Ardhi.
Hayo yamesemwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dkt Hussein Ali Mwinyi katika hafla ya uzinduzi wa mradi wa Mfumo wa usimamizi na usajili wa Ardhi ( LARIS ) uliofanyika Kigunda Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Amesema kupitia mfumo wa LARIS mafanikio makubwa yatapatikana ikowemo kuimarisha uwezo wa Serikali katika kupanga matumizi bora ya ardhi, kuondoa migogoro mbali mbali ya ardhi, kurahisisha upatikanaji wa taarifa sahihi za ardhi, kutambua mipaka na umiliki wa ardhi pamoja na kuongeza imani kwa wawekezaji kwa kupunguza muda wa ushughulikiaji wa maombi yao.
Mhe. Hemed amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeanzisha Shirika la Mawasiliano Zanzibar chini ya sheria namba 4 ya mwaka 2023 vile vile kuanzisha Mamlaka ya Serikali mtandao Zanzibar chini ya sheria namba 1 ya mwaka 2024 kwa lengo la kuweka misingi imara ya kisheria katika usimamizi wa matumizi ya uwekaji wa miundombinu ya TEHAMA na utoaji wa huduma bora na za kisasa kwa wananchi.
Sambamba na hayo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewataka viongozi na wananchi hususan viongozi wa Serikali za Mitaa kusaidia kutoa uelewa kwa wananchi juu ya uwepo wa mradi wa LARIS ili waweze kutoa mashirikiano kwa Wizara ya Ardhi katika kufanikisha utekelezaji wa mradi huo kwa kiwango kilichokusudiwa.
Hata hivyo, ameendelea kuwakumbusha wananchi kuwa amani na mshikamano ndio nguzo muhimu ya maendeleo ambapo bila ya Amani hakuna maendeleo yatakayofikiwa nchini.
Nae Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makaazi Zanzibar Mhe. RAHMA KASSIM ALI amesema Mfumo wa LARIS ni muarobaini wa migogoro ya ardhi ambayo imekuwa ikiongezeka kwa kasi kutokana na wananchi kutokuwa na uwelewa mzuri wa masuala ya Ardhi.
Mhe. Rahma amesema mradi huo utakuwa na faida nyingi ikiwemo mpangilio mzuri wa ardhi utakao ongeza thamani ya Ardhi pamoja na kuongezeka kwa wawekezaji kutokana na kupungua kwa migogoro ya Ardhi.
Aidha Mhe. Rahma amewashauri wananchi kufika Kamisheni ya Ardhi ama kuonana na wataalamu wa masuala ya ardhi ili kuweza kupatiwa taaluma kabla ya kuuziana ardhi jambo litakalo punguza migogoro ya ardhi nchini.
Akiwasilisha taarifa ya Kitaalamu juu ya ujenzi wa Mradi wa LARIS Katibu Mtendaji Kamisheni ya Ardhi ndugu MUSSA KOMBO BAKARI amesema mradi huo ni mihimu katika maendeleo ya sekta ya ardhi ambao utaenda kuleta mabadiliko makubwa katika utatuzi wa changamoto mbali mbali za ardhi.
Ndugu BAKARI amefahamisha kuwa Mkataba wa kitaalamu wa Mradi wa LARIS umefungwa baina ya Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi na Kampuni ya IGNFI kutoka nchini Ufaransa ambao umegharimu zaidi ya URO Milioni 43 ambapo utekelezaji wa mradi huo ni Miezi 24 na miezi 24 mengine ya matengenezo na uendelezaji wa mfumo wa ardhi.
Ameeleza kuwa utekelezaji wa mradi huo utajumuisha maeneo tisa ( 9 ) miongoni mwa hayo ni
Kituo cha taarifa za ardhi, rejea halisi za Vipimo vya Upimaji, uandaaji wa taarifa za Msingi za Kijiografiya na ardhi pamoja na usimamizi wa mabadiliko na kuwajengea uwezo watendaji katika utambuzi na usajili wa Ardhi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya IGNF Bibi AURELIE MILLEDROGUES amesema mradi wa LARIS umeangalia mbali zaidi katika kufanya kazi kwa uwazi, haki na usawa hasa katika utatuzi wa changamoto mbali mbali za ardhi lakini pia kuboresha upatikanaji wa huduma kwa wananchi.
AURELIE amesema mradi huo utafanya kazi kidijitali kwa kuzingatia usalama wa uhifadhi wa taarifa muhimu za masuala ya Ardhi na kuweka kumbukumbu sawa ambazo zitatumika kwa muda mrefu

.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)
No comments