Breaking News

WAKULIMA WA MWANI WATAKIWA KUONGEZA THAMANI MAZAO YAO ILI KUPATA BIDHAA BORA.

 

Na Said Khamis
Wakulima wa mwani Zanzibar wametakiwa kuwa wabunifu katika kuongeza thamani ya zao la mwani mbichi ili kuboresha bidhaa zinazotokana na zao hilo.
 
Hayo ameyasema Kaimu  Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya utafiti wa uvuvi na maliasili za baharini Zanzibar ZAFIRI Ali Saidi Ali  wakati akifungua mafunzo kwa wakulima wa zao la mwani, yenye lengo la kuwajengea uwezo wa kutumia mbinu mbalimbali za kuboresha bidhaa zinazotokana na zao hilo huko ZAFIRI Maruhubi.


 
Amesema hatua hiyo ni muhimu katika kuboresha sekta ya mwani  na kupanua tija katika soko la mwani ndani na nje ya nchi.
 
Aidha amewaomba wakulima wa zao hilo kuyatumia mafunzo waliyopatiwa pamoja na kuwa mabalozi wazuri kwa wakulima wengine.
 
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Alga Seaweed nchini Ireland  Anne Hollier Ruddy amesema lengo kuu ni kuwapa maarifa wakulima hao katika kuongeza thamani ya mwani mbichi na kubuni bidhaa mbalimbali zinazoweza kuuzwa katika masoko ya ndani na nje ya nchi. 


 
Ameongeza kuwa baada ya mafunzo hayo, kutakuwa na hatua nyingine za kuwawezesha wakulima kuendeleza ujuzi walioupata.
 
Nae Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Ethical Seafood Research ESR Abdulrahmani Banisheyba amesema shirika hilo  limejikita katika kuendeleza ufugaji na kilimo cha mazao ya baharini na kutekeleza mpango mkakati wa miaka 13 kwa maendeleo ya sekta ya baharini Zanzibar, ukiwa na lengo la kuimarisha mnyororo wa thamani wa mazao ya baharini na kuongeza manufaa kwa wananchi.


 
Wakulima walioshiriki mafunzo hayo wameeleza kufurahishwa na elimu waliyoipata, huku wakisema imewaongezea uelewa kuhusu njia za kuongeza thamani ya zao la mwani.
Sambamba na hayo wametoa shukrani kwa Serikali na wadau wa maendeleo kwa kuandaa mafunzo hayo ambayo yatachangia kukuza sekta ya mwani na kuinua kipato chao.


Mafunzo hayo siku moja yaliandaliwa na Taasisi ya utafiti wa uvuvi na maliasili za baharini Zanzibar ZAFIRI kwa kushirikiana na Kampuni ya Alga Seaweed Limited pamoja na Shirika la Ethical Seafood Research(ESR).

1 comment: