JUNI 17 NI SIKU YA MAPUMZIKO ZANZIBAR, KUUKARIBISHA MWAKA MPYA WA KIISLAMU 1448 HIJRIA : RAIS DKT MWINYI
Na Said Khamis
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ametangaza kuwa Jumatano, tarehe 17 Juni 2026, itakuwa siku ya mapumziko rasmi Zanzibar kwa ajili ya kuukaribisha Mwaka Mpya wa Kiislamu 1448 Hijria.
Tangazo hilo limetolewa leo kupitia Ikulu Zanzibar, likieleza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya kutambua na kuadhimisha mwanzo wa mwaka mpya wa Kiislamu, ambao ni miongoni mwa siku muhimu kwa Waislamu na wananchi wa Zanzibar kwa ujumla.
Katika tamko hilo, Dkt. Mwinyi amesema siku hiyo itatoa nafasi kwa wananchi, hususan waumini wa dini ya Kiislamu, kuukaribisha mwaka mpya kwa ibada, dua na matendo mema, huku wakimuomba Mwenyezi Mungu aendelee kuijalia Zanzibar na Tanzania amani, umoja na ustawi.
Aidha, Rais Mwinyi amewahimiza wananchi kuitumia fursa ya mwanzo wa mwaka mpya kujitathmini, kuimarisha uchamungu, kusaidiana na kuendeleza maadili mema yanayochangia mshikamano wa familia na maendeleo ya Taifa.
Amesisitiza umuhimu wa kuendeleza misingi ya maadili, upendo na mshikamano katika jamii ili kudumisha amani na maendeleo yanayopatikana nchini.
Vilevile, taasisi za Serikali, sekta binafsi, waajiri na wananchi wote wametakiwa kuzingatia tangazo hilo kwa kufuata taratibu zilizowekwa kuhusu siku ya mapumziko.
Akihitimisha ujumbe wake, Rais Dkt. Mwinyi amewatakia Waislamu na wananchi wote wa Zanzibar heri ya Mwaka Mpya wa Kiislamu 1448 Hijria, akiomba mwaka huo uwe wa kheri, afya njema, mafanikio na maendeleo kwa wote.

No comments