Breaking News

WAFANYA BIASHARA PEMBA WATAKIWA KUSHIRIKIANA NA ZFDA KULINDA USALAMA WA CHAKULA.

Na mwandishi wetu Pemba.

 Wafanyabiashara wadogo wadogo na wajasiriamali wanaofanya biashara katika eneo la Bandari ya Mkoani, Pemba, wametakiwa kushirikiana kwa karibu na Ofisi ya Wakala wa Chakula, Dawa na Vipodozi Zanzibar (ZFDA) kwa kutoa taarifa za bidhaa zilizopitwa na muda wa matumizi ili kusaidia kulinda afya za wananchi.

Wito huo umetolewa na Kaimu Mkurugenzi wa ZFDA Pemba, Abdalla Shariff Maalim, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Usalama wa Chakula Duniani yaliyofanyika katika Bandari ya Mkoani, ambapo alisisitiza kuwa usalama wa chakula ni jukumu la kila mwananchi na mdau wa biashara.

Abdalla alisema wafanyabiashara wana nafasi muhimu katika kusaidia mamlaka husika kubaini na kuondoa bidhaa zisizo salama kabla hazijawafikia walaji. Alieleza kuwa ni muhimu kwa wafanyabiashara kutoa taarifa mara wanapobaini uwepo wa bidhaa zilizopitwa na muda wa matumizi ili hatua za haraka zichukuliwe kwa manufaa ya jamii.



Kwa upande wao, maafisa wa ZFDA walieleza kuwa taasisi hiyo ina wajibu wa kusimamia ubora na usalama wa chakula katika hatua zote za mnyororo wa uzalishaji na usambazaji. Walisema usimamizi huo unahusisha utayarishaji, uhifadhi, usafirishaji na usambazaji wa chakula hadi kumfikia mlaji wa mwisho kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo iliyowekwa.



Maafisa hao waliongeza kuwa ushirikiano wa wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla ni nguzo muhimu katika kuhakikisha bidhaa zinazouzwa sokoni zinakidhi viwango vya usalama na ubora vinavyotakiwa.

Hata hivyo, baadhi ya wafanyabiashara waliohudhuria maadhimisho hayo walieleza kuwa bado wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa uelewa kuhusu sehemu sahihi za kuwasilisha taarifa wanapobaini bidhaa zisizo salama au wafanyabiashara wanaokiuka taratibu za biashara.





Walisema hali hiyo wakati mwingine husababisha hasara katika biashara zao na kuomba ZFDA pamoja na taasisi nyingine husika kuendelea kutoa elimu zaidi kuhusu taratibu za utoaji wa taarifa na namna ya kushiriki katika kulinda usalama wa chakula.

Maadhimisho ya Siku ya Usalama wa Chakula Duniani yamekuwa fursa muhimu ya kuongeza uelewa kwa wafanyabiashara na wananchi kuhusu umuhimu wa kuhakikisha chakula kinachozalishwa, kusafirishwa, kuhifadhiwa na kuuzwa ni salama kwa matumizi ya binadamu, hivyo kuchangia afya bora na maendeleo ya jamii.


No comments