Breaking News

VIJANA WA ZANZIBAR WANUFAIKA NA MAFUNZO YA UJASIRIAMALI KUPITIA SMZ NA CHUO KIKUU CHA KILIMO CHA CHINA

 


Na Mwandishi Wetu.

USHIRIKIANO kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Chuo Kikuu cha Kilimo cha China (China Agricultural University - CAU) umeendelea kuzaa matunda baada ya vijana wajasiriamali kutoka Zanzibar kunufaika na mafunzo mbalimbali yanayolenga kuimarisha uwezo wao katika sekta za kilimo, viwanda, utalii na uchumi wa buluu.

Ujumbe wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha China ulioongozwa na Profesa Xi Jin ulifanya ziara maalumu kutembelea miradi inayotekelezwa na washiriki wa programu ya kuwawezesha vijana wa vijijini kuingia katika shughuli za ujasiriamali. Profesa Xi alisema lengo kuu la programu hiyo ni kuwawezesha vijana kupitia elimu, teknolojia za kisasa na mbinu za ujasiriamali zitakazowasaidia kubadilisha maisha yao pamoja na jamii zinazowazunguka.

Katika ziara hiyo, ujumbe ulitembelea maeneo mbalimbali ikiwemo Viwanda Dunga Zuze, Madrasa Abdulrahman Buyu, shamba la mboga mboga Bungi, miradi ya kilimo na ufugaji pamoja na maeneo ya utalii Fumba. Profesa Xi alisisitiza kuwa vijana ni nguzo muhimu katika maendeleo ya vijijini, hivyo wanahitaji kupewa maarifa, teknolojia na fursa zinazoweza kuwawezesha kuleta mabadiliko chanya katika sekta za uzalishaji na huduma.



Alieleza kuwa programu hiyo pia inalenga kujenga mtandao wa vijana wajasiriamali kutoka Zanzibar, Afrika na nchi nyingine za Kusini mwa Dunia (Global South), ili kuwapa fursa ya kubadilishana uzoefu, kupata ushauri kutoka kwa wataalamu na kunufaika na mafunzo pamoja na fursa za ufadhili kwa ajili ya kukuza biashara zao.

Akizungumza kuhusu utekelezaji wa mradi huo, Ofisa Mkuu wa Miradi ya Maendeleo ya Viwanda kutoka Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar, Yahya Khatibu Haji, alisema mradi huo ulizinduliwa rasmi tarehe 4 Agosti 2024 na aliyekuwa Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda, Mhe. Omar Said Shaaban.

Alifafanua kuwa mradi huo unawalenga vijana wanaojihusisha na kilimo, viwanda, utalii na uchumi wa buluu kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kuanzisha na kukuza biashara endelevu zinazoweza kuchangia maendeleo ya kiuchumi nchini.



Kwa mujibu wa Yahya Khatibu Haji, awamu ya kwanza ya programu hiyo iliwahusisha vijana 20 kutoka Tanzania na Uganda, huku awamu ya pili inayojulikana kama Global South Rural Initiative for Entrepreneurs ikipanua wigo wa washiriki kutoka nchi mbalimbali zinazoendelea.



Kwa upande wao, washiriki wa programu hiyo akiwemo Amina Salum na Ilham Said Omar, kwa niaba ya wenzao, walieleza kuwa mafunzo waliyopata yamewasaidia kuongeza ujuzi wa kuendesha biashara za utalii na kuboresha uzalishaji wa mazao ya mboga mboga kwa kutumia teknolojia za kisasa zinazorahisisha usimamizi wa mazingira ya kilimo.





Mpango huo unatarajiwa kuendelea kuwa chachu ya maendeleo kwa vijana wa Zanzibar kwa kuwapatia maarifa, mitandao ya kimataifa na fursa za kujikwamua kiuchumi kupitia ujasiriamali unaozingatia ubunifu na matumizi ya teknolojia za kisasa.


No comments