TAMWA ZANZIBAR YAZINDUA MRADI WA W-LEAD KUIMARISHA UONGOZI WA WANAWAKE VIJANA ZANZIBAR.
Na Safia Mohamed.
Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania Zanzibar (TAMWA-ZNZ) kimezindua rasmi mradi wa Women Leaders for Equality, Accountability and Democracy (W-LEAD) unaolenga kuongeza ushiriki wa wanawake, hususan wanawake vijana na wanawake wenye ulemavu, katika nafasi za uongozi na mifumo ya maamuzi Zanzibar. Uzinduzi wa mradi huo unakuja wakati ambapo wanawake wanaendelea kukabiliwa na changamoto mbalimbali zinazowazuia kushiriki kikamilifu katika uongozi licha ya kuwa asilimia 51 ya wakazi wa Zanzibar kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022.
Akizungumza kuhusu mradi huo, Mkurugenzi wa TAMWA Zanzibar, Nairat Abdulla Ali, alisema kuwa wanawake viongozi Zanzibar bado ni asilimia 38 pekee, hali inayodhihirisha uwepo wa pengo kubwa la uwakilishi ikilinganishwa na wanaume. Alieleza kuwa changamoto za kijamii, kiuchumi na kiutamaduni zimechangia kwa muda mrefu kuwafanya wanawake na wasichana kukosa fursa sawa za kushiriki katika uongozi na kufanya maamuzi.
Kupitia mradi wa W-LEAD, wanawake 100 watapatiwa mafunzo ya uongozi, ushiriki wa kidemokrasia na stadi za kujiamini ili kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika nafasi mbalimbali za maamuzi. Aidha, wanawake vijana 60 wataunganishwa na taasisi za umma, sekta binafsi na asasi za kiraia kwa ajili ya kupata uzoefu wa vitendo katika masuala ya uongozi, utawala bora na usimamizi wa taasisi.
Mradi huo pia unatarajia kuwafikia zaidi ya wananchi 100,000 kupitia kampeni za kuhamasisha usawa wa kijinsia na kuondoa mitazamo inayokwamisha ushiriki wa wanawake katika uongozi. Lengo ni kujenga jamii inayotambua na kuunga mkono ushiriki sawa wa wanawake na wanaume katika michakato ya maendeleo na maamuzi.
Sambamba na hilo, asasi tano za kiraia na vyama vitatu vya siasa vitawezeshwa kuandaa sera na mifumo inayozingatia usawa wa kijinsia. Pia watetezi 60 wa haki za wanawake watajengewa uwezo wa kufuatilia na kushughulikia matukio ya ukatili dhidi ya wanawake, huku waandishi wa habari 30 wakipatiwa mafunzo ya kuripoti kwa weledi masuala ya wanawake na uongozi.
Afisa Ufuatiliaji na Tathmini mohammed khatib mohammed amesema vijana kutoka asasi za kiraiya watawezeshwa kujiamini na kutoa elimu zaidi kwa vana wenzao waweze kujitokeza kufuatilia nafasi mbali mbali za uongozi hususan wanawake na watoto wa kike.
Mradi wa W-LEAD unatekelezwa na TAMWA Zanzibar kwa ushirikiano na Jumuiya ya Wasioona Zanzibar (ZANAB), State University of Zanzibar (SUZA) na Zanzibar University. Mradi huo unafadhiliwa na European Union kupitia mpango wa Women and Youth Democratic Engagement (WYDE) na utatekelezwa kuanzia mwaka 2026 hadi 2027 ukiwa na kauli mbiu isemayo: “Kujenga Zanzibar ambayo wanawake na wanaume wanashiriki kwa usawa katika kuunda na kuendeleza jamii zenye demokrasia na ujumuishi kwa wote.”
No comments