MWANAMKE INTIATIVE FOUNDATION INA MCHANGO MKUBWA KIELIMU. '' MKUU WA MKOA KUSINI''
Na Safia Mohammed.
MKUU wa Mkoa wa Kusini Unguja, Hamida Mussa Khamis, ameipongeza Taasisi ya Mwanamke Initiative Foundation (MIF) kwa mchango wake mkubwa katika kuimarisha sekta ya elimu nchini.
Akizungumza katika hafla iliyofanyika Skuli ya Kibele, Hamida amesema kuwa kuwepo kwa mikakati imara ya Serikali pamoja na mazingira wezeshi kwa taasisi zisizo za kiserikali kumesaidia wadau wa elimu kushiriki kikamilifu katika kutatua changamoto zinazoikabili sekta hiyo.
Hafla hiyo imewakutanisha walimu wakuu, wenyeviti wa kamati za skuli pamoja na wadau mbalimbali wa elimu, ikiwa na lengo la kuipongeza MIF kwa mchango wake katika kuunga mkono juhudi za Serikali na kuwazawadia vyeti walimu waliofanya vizuri katika masomo ya Sayansi, Lugha na Sayansi Jamii.
Mkuu huyo amesema ndani ya kipindi cha miaka mitano iliyopita, MIF imeonyesha dhamira ya dhati ya kuleta mageuzi katika elimu kupitia utekelezaji wa miradi na programu mbalimbali zinazolenga kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia.
Ameeleza kuwa miradi hiyo imekuwa ikitafuta suluhisho la changamoto zinazochangia kushuka kwa kiwango cha elimu, ikiwemo udhaifu wa ufaulu katika baadhi ya masomo na ukosefu wa hamasa kwa wanafunzi na walimu.
Hamida, amesema juhudi hizo zimeanza kuzaa matunda kwa kuongezeka kwa hamasa ya kujifunza na kufundisha katika skuli nyingi za Mkoa wa Kusini Unguja, hali ambayo imechangia kuboreka kwa matokeo ya wanafunzi katika mitihani mbalimbali.
Aidha, amesema Serikali ya Mkoa wa Kusini Unguja itaendelea kuimarisha sekta ya elimu kwa kuweka mikakati madhubuti itakayosaidia kupunguza idadi ya wanafunzi wanaopata matokeo ya sifuri na hatimaye kutokomeza kabisa tatizo hilo.
Amebainisha kuwa lengo jingine ni kuongeza idadi ya wanafunzi wanaofaulu kwa madaraja ya kwanza na pili, huku akisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali, walimu, wazazi na wadau wa maendeleo katika kufanikisha azma hiyo.
Kwa upande wake, mwakilishi wa MIF, Fahmi Ali Mwinyi, amesema taasisi hiyo itaendelea kutekeleza programu mbalimbali za maendeleo ya elimu kutokana na kutenga sehemu kubwa ya bajeti yake ya mwaka huu kwa ajili ya kusaidia shughuli za kuboresha ufaulu na ubora wa elimu.
Amesema MIF inaamini kuwa elimu bora ndiyo msingi wa maendeleo endelevu ya jamii, hivyo itaendelea kushirikiana na Serikali pamoja na wadau wengine kuhakikisha wanafunzi wanapata mazingira bora ya kujifunzia na kufikia malengo yao ya kitaaluma.
Naye Ofisa Elimu Mkoa wa Kusini Unguja Mussa Nahodha Makame alisema mafanikio yanayoonekana hivi sasa ni matokeo ya ushirikiano mzuri kati ya Serikali na taasisi za maendeleo, akieleza kuwa mchango wa MIF umekuwa chachu ya kuimarika kwa kiwango cha elimu katika mkoa huo.
Akizungumza katika hafla hiyo Ofisa Elimu Wilaya ya Kusini Unguja Khamis Mcha Khamis aliishukuru MIF kwa kuendelea kusaidia juhudi za Serikali katika sekta ya elimu na kuahidi kuwa ushirikiano uliopo utaendelezwa ili kuhakikisha mafanikio yaliyopatikana yanaimarika zaidi mwaka hadi mwaka kwa manufaa ya wanafunzi na taifa kwa ujumla.

No comments