Breaking News

WANANDOA WATAKIWA KUANDIKISHIANA MALI KUEPUSHA MIGOGORO.



Wanandoa wametakiwa kuandikishiana mali wanapopeana au kukopeshana ili kuepusha migogoro inayoweza kujitokeza pindi kunapovunjika kwa mahusiano yao. Wito huo umetolewa katika mafunzo ya elimu ya sheria yaliyofanyika katika kijiji cha Kikungwi, Wilaya ya Kati, Unguja, yakilenga kuwaongezea wananchi uelewa kuhusu haki zao za kisheria.

Akizungumza katika mafunzo hayo, mkufunzi Dk. Sikujua Omar Hamdan alisema ni jambo la kawaida kwa wanandoa kupeana mali bila kuweka kumbukumbu rasmi, hali ambayo huleta matatizo makubwa baadaye pindi wanapotofautiana.

Alisema mara nyingi wanandoa wanapokuwa katika uhusiano mzuri hupeana mali kwa kuaminiana, lakini wanapokuja kuachana huzuka migogoro mikubwa, hasa kwa upande wa wanawake ambao hukosa ushahidi wa kudai haki zao.

Aidha, alifafanua kuwa wanawake wengi hushindwa kudai haki zao kutokana na kukosa vielelezo vinavyothibitisha umiliki au makubaliano ya mali waliyopewa au kukopeshana na wenza wao.

Alisisitiza kuwa ili sheria iweze kumsaidia mtu kudai haki yake, ni muhimu kuwepo kwa ushahidi wa maandishi unaothibitisha makubaliano hayo, huku akieleza kuwa kuandikishiana mali siyo ishara ya kutokuaminiana bali ni njia ya kujilinda kisheria.

Kwa upande wake, Mratibu wa Programu kutoka Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar (ZLSC), Denis Rwekamwa Joseph, alisema kituo hicho kinatoa msaada wa kisheria kwa wananchi wanaokumbana na changamoto mbalimbali, na kuwahimiza wananchi kutumia huduma hizo wanapohitaji ushauri.

Alieleza kuwa huduma hizo zinalenga kusaidia jamii kupata haki zao kwa wakati na kwa njia sahihi, huku akisisitiza umuhimu wa wananchi kufika katika kituo hicho mapema wanapokumbana na matatizo ya kisheria badala ya kukaa kimya.

Nao baadhi ya wananchi walioshiriki mafunzo hayo, walisema elimu hiyo imewasaidia kuelewa haki zao na umuhimu wa kufuata taratibu za kisheria, jambo litakalosaidia kupunguza migogoro isiyo ya lazima katika jamii.


No comments