Breaking News

SERIKALI YAENDELEA NA OPERESHENI YA KUKAMATA WANYAMA WANAOZURURA MJINI

Na Fatma Rajab

Serikali imesema itaendelea na operesheni ya kukamata wanyama wanaozurura ovyo katika maeneo ya mjini, ikiwa ni hatua ya kulinda usalama wa wananchi pamoja na kuhakikisha mazingira yanabaki safi na yenye mpangilio mzuri.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Mjini, Dk. Said Haji Mrisho, alipokuwa akisimamia zoezi la ukamataji wa wanyama hao, ambapo alisisitiza kuwa ufugaji ndani ya maeneo ya mjini haukubaliki na ni kinyume cha sheria zilizowekwa.

Alieleza kuwa kuwepo kwa wanyama wanaozurura ovyo kunachangia kwa kiasi kikubwa ajali za barabarani pamoja na uchafuzi wa mazingira, hali inayohatarisha afya na usalama wa wananchi wanaoishi katika maeneo hayo.

“Hatutavumilia uvunjifu wa sheria hii, tunataka kuona kila mwananchi anachukua jukumu la kuhakikisha mji unabaki salama, safi na wenye utaratibu,” alisema Dk. Mrisho.

Aidha, alibainisha kuwa operesheni hiyo haitakuwa ya muda mfupi bali itaendelea kwa kipindi kirefu, hadi pale tatizo la wanyama kuzurura ovyo litakapodhibitiwa kikamilifu katika maeneo yote ya mjini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Manispaa ya Mjini, Hasina Attai Masoud, alisema operesheni hiyo ni sehemu ya jitihada endelevu za kudhibiti ufugaji holela, huku akionya kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watakaokiuka agizo hilo.

Masoud alisisitiza kuwa miji imekusudiwa kuwa maeneo ya makazi na biashara, hivyo ni muhimu wananchi kuheshimu mipaka ya matumizi ya ardhi na kuacha mara moja kufuga wanyama katika maeneo yasiyoruhusiwa.

Baadhi ya wananchi waliopata nafasi ya kuzungumza walieleza kuridhishwa na hatua hiyo, wakisema imekuwa kero kuona wanyama wakizurura barabarani, huku katika operesheni hiyo maofisa wa manispaa wakifanikiwa kukamata mbuzi sita waliokuwa wakizurura ovyo katika mitaa ya mjini.


No comments