Breaking News

TAMWA-ZNZ YAWAWEZESHA WAFANYAKAZI WA SEKTA ISIYO RASMI KUKABILIANA NA UKATILI WA KIJINSIA


Na Said khamis.

Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Zanzibar (TAMWA-ZNZ) kimeandaa mafunzo maalum kwa viongozi na wafanyakazi wa sekta isiyo rasmi kutoka Wilaya ya Kaskazini A, Unguja, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kupambana na udhalilishaji na ukatili wa kijinsia katika jamii.

Mafunzo hayo yamewakutanisha wadau mbalimbali wakiwemo wafanyakazi wa masokoni, mama ntilie, wanikaji wa dagaa, wakulima wa mwani, wavunaji wa majongoo bahari, wavuvi, manahodha, wafanyabiashara ndogo ndogo pamoja na wakulima wa muhogo na ndizi, kwa lengo la kuwajengea uelewa na uwezo wa kukabiliana na changamoto zinazowakabili katika maeneo yao ya kazi na maisha ya kila siku.

Akifungua mafunzo hayo, Mkuu wa Maafisa Programu kutoka TAMWA-ZNZ, Zaina Abdalla Mzee, amesema kuwa udhalilishaji na ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na wasichana ni janga la kidunia linalokiuka haki za binadamu, na kusisitiza kuwa kila mtu ana wajibu wa kushiriki katika kupinga vitendo hivyo.

“Ni muhimu kwa kila mmoja wetu kuchukua hatua za makusudi kuhakikisha tunajiepusha na kushiriki katika vitendo vya udhalilishaji na ukatili, pamoja na kulinda haki za wanawake na watoto,” amesema Zaina.



Kwa upande wake, Afisa Programu wa TAMWA-ZNZ, Asia Hakim Makame, amesema kuwa mafunzo hayo yanalenga kuwajengea washiriki uelewa kuhusu aina mbalimbali za ukatili wa kijinsia unaoweza kutokea katika maeneo yao ya kazi, njia sahihi za kuripoti matukio hayo, pamoja na kutambua haki zao kama wafanyakazi.

Ameongeza kuwa kupitia mafunzo hayo, washiriki watawezeshwa kujenga mazingira salama na yenye usawa, huku wakihamasishwa kushiriki kikamilifu katika kupinga vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na wasichana katika jamii zao.



Mkufunzi wa mafunzo hayo, ambaye pia ni mwanaharakati wa kupambana na ukatili wa kijinsia, Sabahi Bakar Hassan, amesema kuwa vitendo vya udhalilishaji vinaweza kumtokea mtu yeyote bila kujali jinsia au umri, lakini wanawake na wasichana wako katika hatari zaidi kutokana na mila na desturi potofu zilizojengeka katika jamii.

Amesisitiza kuwa ukosefu wa uwajibikaji katika mifumo ya utoaji haki huchangia kuendelea kwa vitendo hivyo, na kutoa wito wa kuimarishwa kwa ushirikiano kati ya sekta mbalimbali na jamii kwa ujumla ili kukabiliana na changamoto hiyo.

Washiriki wa mafunzo hayo wameeleza dhamira yao ya kuwa mabalozi wa mabadiliko katika jamii, kwa kuhakikisha wanapinga na kukemea vitendo vya ukatili wa kijinsia katika maeneo yao ya kazi na makazi.



Mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa Mradi wa “Tunaweza Pamoja” unaotekelezwa na UN Women kwa kushirikiana na TAMWA Zanzibar, kwa ufadhili wa Serikali ya Norway chini ya mpango wa pamoja wa Umoja wa Mataifa, unaolenga kujenga jamii salama, yenye usawa na isiyovumilia ukatili dhidi ya wanawake na wasichana.


No comments