TAMWA-ZNZ YAJA KIVYENGINE YAONGEZA NGUVU SEKTA YA USAFIRISHAJI, MAPAMBANO DHIDI YA UDHALILISHAJI WA KIJINSIA.
Na Fatma Rajab.
Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania Zanzibar (TAMWA-ZNZ) kimetoa mafunzo maalum ya siku moja kwa watoa huduma za usafirishaji wa umma kutoka Wilaya ya Kaskazini A, Unguja, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha mapambano dhidi ya udhalilishaji na ukatili wa kijinsia katika sekta ya usafirishaji visiwani Zanzibar.
Lengo la mafunzo hayo ni
kuwajengea uelewa na kuwashirikisha watoa huduma wa usafiri usio rasmi katika
kuzuia na kupambana na vitendo vya ukatili na udhalilishaji dhidi ya wanawake
na watoto wa kike, pamoja na kuhakikisha wanawake na wasichana wanapata huduma
za usafiri katika mazingira salama na yenye heshima.
Akizungumza katika mafunzo
hayo yaliyofanyika katika Ukumbi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Mkokotoni, Afisa
Programu kutoka TAMWA-ZNZ, Asia Hakim Makame, amesema mafunzo hayo yataongeza
uwajibikaji kwa watoa huduma za usafiri, kubadili mitazamo hasi kuhusu wanawake
na kusaidia kuifanya sekta ya usafiri kuwa sehemu salama kwa wanawake
wanaotumia usafiri huo na jamii.
Amesema kupitia mafunzo hayo,
washiriki wameshirikishwa kuandaa na kukubaliana kwa pamoja Kanuni ya Maadili
(Code of Conduct) itakayowaongoza katika utoaji wa huduma kwa kuzingatia
misingi ya heshima, usalama na uwajibikaji.
“Kanuni hiyo inalenga
kuhakikisha wanawake na wasichana wanaheshimiwa, kuzuia vitendo vya unyanyasaji
wa kijinsia, matumizi ya lugha chafu na vitisho, kulinda usalama wa abiria
wakati wa safari, pamoja na kuripoti matukio ya ukatili au udhalilishaji
yatakayoshuhudiwa,” amesema Asia.
Aidha, amesema hatua hiyo
itasaidia kujenga mazingira salama na rafiki kwa wanawake na watoto wa kike
wanapotumia vyombo vya usafiri wa umma.
Kwa upande wake, mtoa mada
kuhusu mabadiliko ya kitabia kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee
na Watoto Zanzibar, Mohamed Jabir Makame, amesema baadhi ya vitendo vya
udhalilishaji katika sekta ya usafiri husababishwa na ukosefu wa elimu kuhusu
heshima, maadili na nidhamu kwa watoa huduma.
Amesema elimu hiyo
itawasaidia watoa huduma kutambua vitendo vya ukatili wa kijinsia na kuepuka
kuvifanya kwa makusudi au bila kutambua madhara yake kwa jamii.
Washiriki wa mafunzo hayo
wameeleza kuwa changamoto ya udhalilishaji katika sekta ya usafiri ipo kwa
pande zote mbili kati ya dereva na abiria, hivyo wamependekeza elimu hiyo
kuendelea kutolewa kwa jamii nzima ili kuongeza uelewa na kujenga mahusiano
yenye kuheshimiana.
Washiriki hao pia wameahidi
kuwa mabalozi wa kupinga ukatili wa kijinsia na kulinda usalama wa wanawake na
wasichana katika maeneo yao ya kazi na jamii kwa ujumla.
Mafunzo hayo yamewakutanisha wadau mbalimbali wakiwemo waendesha bodaboda, , madereva wa magari ya abiria, madereva wa bajaji, askari wa usalama barabarani pamoja na Afisa Takwimu kutoka Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Mafunzo hayo ni sehemu ya
utekelezaji wa Mradi wa “Tunaweza Pamoja” unaotekelezwa na UN Women kwa
kushirikiana na TAMWA Zanzibar kwa ufadhili wa Serikali ya Norway chini ya mpango
wa pamoja wa Umoja wa Mataifa unaolenga kujenga jamii salama, yenye usawa na
isiyovumilia ukatili dhidi ya wanawake na wasichana.


.jpeg)


No comments