Breaking News

DC KATI AWAASA MAMA WAJAWAZITO KUWAHI KLINIKI MAPEMA KUPATA HUDUMA



Mkuu wa Wilaya ya Kati, Rajab Ali Rajab, amewataka wanawake wajawazito kuhakikisha wanahudhuria kliniki mapema mara tu wanapogundua kuwa na ujauzito ili kupata huduma za afya kwa wakati na kuepuka madhara yanayoweza kuhatarisha maisha yao pamoja na watoto wao.

Akizungumza katika kikao cha tathmini na uhamasishaji wa masheha kilichofanyika Dunga, Wilaya ya Kati Unguja, Rajab alisema bado kuna changamoto ya baadhi ya wajawazito kuchelewa kufika vituo vya afya, hali inayochangia kuongezeka kwa matatizo wakati wa ujauzito na kujifungua.

Alieleza kuwa lengo la kikao hicho ni kuwajengea uwezo masheha juu ya umuhimu wa kuwa na takwimu sahihi za kuripoti vifo vitokanavyo na uzazi, hususan kwa kina mama wanaojifungulia majumbani bila kufika hospitalini.

“Ni muhimu kwa mama mjamzito kuwahi kliniki ili madaktari waweze kufuatilia maendeleo ya afya yake na ya mtoto tangu mwanzo wa ujauzito, endapo kutakuwa na changamoto yoyote, hatua za matibabu zitachukuliwa mapema,” alisema Rajab.

Aliongeza kuwa Serikali imeendelea kuimarisha huduma za afya ya mama na mtoto kwa kujenga na kuboresha vituo vya afya mijini na vijijini, jambo ambalo limeongeza upatikanaji wa huduma karibu na wananchi.

Rajab alisema matumizi sahihi ya huduma hizo yatachangia kupunguza vifo vya mama na mtoto vinavyotokana na uzazi, huku akiwasisitiza wananchi kuachana na tabia ya kujifungulia majumbani bila usimamizi wa wataalamu wa afya.

Aidha, aliwataka masheha kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa kujifungulia hospitalini pamoja na kushirikiana na watendaji wa afya katika kuimarisha utoaji wa huduma wilayani humo.

Kwa upande wake, Daktari zamana wa Wilaya ya Kati, Amina Hussein Pandu, alisema licha ya Serikali kusogeza huduma za afya karibu na wananchi, bado baadhi ya wanawake wajawazito hufika hospitalini wakiwa katika hatua za mwisho za ujauzito au wakati matatizo tayari yamejitokeza.

Alisema hali hiyo mara nyingi huwafanya wananchi kuwalaumu madaktari na wauguzi pale matatizo yanapotokea, wakati chanzo kikubwa ni kuchelewa kufika vituoni kwa ajili ya uchunguzi na huduma muhimu za kitabibu.

Akitoa takwimu za afya ya mama na mtoto kwa mwaka 2025 Muuguzi Mkuu na Mratibu wa Huduma za Mama na Mtoto Wilaya ya Kati, Asha Msenga Mrisho, alisema jumla ya vifo 12 vya watoto wachanga viliripotiwa katika kipindi hicho.

Alifafanua kuwa kati ya vifo hivyo, watoto wanane walifariki tumboni, watatu walifariki wakati wa uchungu wa kujifungua na mmoja alifariki baada ya kuzaliwa, huku akieleza kuwa hakuna kifo cha mama kilichoripotiwa katika kipindi hicho.

Hata hivyo alisema kuanzia Januari hadi Machi mwaka huu, wilaya hiyo ilishuhudia vifo viwili vya wajawazito ambapo kifo kimoja kilitokea kituoni na kingine njiani wakati mama mjamzito akipelekwa hospitalini kwa matibabu.

Kwa upande wa watoto wachanga katika kipindi hicho, alisema vifo sita viliripotiwa, ambapo vitatu vilitokea watoto wakiwa tumboni, viwili wakati wa kujifungua na kimoja baada ya mtoto kuzaliwa.

Naye Daktari kutoka Kituo cha Afya Unguja Ukuu, Jabir Zahir Khamis, alisema bado kuna mwitikio mdogo wa wanaume kuwafuatana wenza wao kliniki wakati wa ujauzito.

Alisema ushiriki wa baba tangu mwanzo wa ujauzito hadi wakati wa kujifungua husaidia kuboresha afya ya mama na mtoto pamoja na kugundua changamoto mbalimbali zinazoweza kujitokeza mapema.

Kwa upande wake, Daktari Khadija Mberk Rashid wa Kituo cha Afya Mwera alionya tabia ya baadhi ya wajawazito kutofuata maelekezo ya wataalamu wa afya, akisema hali hiyo inaweza kusababisha kuharibika kwa mimba au kuhatarisha maisha ya mama na mtoto.

Naye Daktari Maryam Omar wa kituo cha Afya chwaka alisema baadhi ya wajawazito bado wana tabia ya kupaka hina, kuchora piko, kufanya kazi nzito na kutumia dawa za mitishamba wanapopata uchungu wa kujifungua, jambo ambalo ni hatari kwa afya yao na watoto wao.

Kwa upande wa masheha walieleza kufurahishwa na hatua za Serikali katika kuboresha huduma za afya, hivyo waliomba kuongeza idadi ya madaktari, wauguzi na wahudumu wa afya katika vituo mbalimbali ili kuongeza ufanisi wa huduma kwa wananchi.

Kikao hicho kiliwashirikisha masheha, madaktari na wauguzi wa vituo vya afya vinavyotoa huduma za uzazi katika Wilaya ya Kati.



1 comment: