JESHI LA POLISI KUIMARISHA ULINZI KIPINDI CHA SIKU KUU.
Na Said Khamis
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi limejipanga kuimarisha hali ya ulinzi na usalama katika maeneo yote ya Mkoa huo ikiwemo maeneo ya ibada, viwanja vya kusherekea watoto pamoja na maeneo mengine ya kijamii ili kuhakikisha sikukuu ya Eidl Adh ha inasherekewa kwa amani na utulivu.
Hayo ameyasema Kaimu Kamanda Mkoa wa Mjini Magharib Kamishna Msaidizi wa Polisi Abubakar Khamis Ali wakati akizungumza na waandishi wa habari huko Afisini kwake Madema Mjini Unguja.
Amesema Katika kipindi chote cha sikukuu, kutakuwa na doria na misako ya mara kwa mara ikihusisha askari wa miguu, magari, pikipiki pamoja na vikosi maalum ikiwemo kikosi cha mbwa na farasi kwa lengo la kudhibiti vitendo vya uvunjifu wa amani.
Pia Jeshi la Polisi limewaasa wananchi kuchukua tahadhari wanapokuwa katika shughuli za sikukuu, hususani wanapotoka majumbani mwao, kuhakikisha wanalinda mali zao, kuepuka kuondoka wote kwa pamoja na kufuatilia kwa karibu mienendo ya watoto wao ili kuepusha vitendo vya kihalifu.
Hata hivyo Kaimu Kamanda huyo ameeleza kuwa katika kuhakikisha usalama na mtiririko mzuri wa shughuli za sikukuu, baadhi ya barabara zitafungwa kwa muda, ikiwemo Barabara ya Ngambo Polisi hadi Kariakoo. Barabara ya Kwa Biziredi hadi Kariakoo. Barabara ya Kibanda Maiti hadi Kariakoo. Barabara ya Round About Miembeni hadi Kariakoo. Barabara ya Maisara hadi Mnazi Mmoja. Barabara ya Baraza la Wawakilishi la zamani hadi Magazeti. Barabara ya kwa Mzee Mwinyi hadi Bosnia.
Aidha, askari wa usalama barabarani watakuwepo kwa wingi katika maeneo mbalimbali ili kudhibiti madereva wazembe na kuhakikisha sheria za usalama barabarani zinafuatwa.
Sambamba na hayo Madereva wote wamesisitizwa kuendesha kwa tahadhari, kuzingatia sheria, kuwa na leseni halali pamoja na kuhakikisha vyombo vyao vimekaguliwa.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi linatoa wito kwa wananchi kusherehekea sikukuu ya Eid Al-adha kwa amani, utulivu na kuzingatia sheria za nchi.
"Sikukuu isiwe chanzo cha vitendo vya uvunjifu wa amani kama wizi, uporaji, unyang’anyi na udhalilishaji" amesema kaimu kamanda
Aidha, Jeshi la Polisi linatoa onyo kali kwa mtu yeyote atakayejihusisha na vitendo vya uvunjifu wa amani au kujipatia kipato kwa njia isiyo halali kuwa, hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake bila kusita.


e bwana wee
ReplyDelete